KAMATI
ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imekagua mradi wa
TANAPA wa ujenzi wa mahema matatu ya kudumu unaogharimu kiasi cha
shilingi milioni 163 katika Hifadhi ya Kisiwa cha Saanane jijini Mwanza.
Akizungumza
katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi,
Maliasili na Utalii, Mhe. Ally Juma Makoa (Mb) amemuelekeza mkandarasi
kuharakisha ujenzi wa mahema hayo ili kuvutia zaidi watalii
wanaotembelea kisiwa hicho.
“Endapo
mahema haya yatakamilika na mkiongeza ubunifu wa kukitangaza kisiwa
hiki kwa kutumia watu maarufu, lengo la kuongeza mapato yatokanayo na
utalii litatimia,”amesema Mhe. Makoa.
Aidha, amewataka watendaji wa hifadhi hiyo kupima uwekezaji wa mahema hayo kama utarudisha fedha zilizotolewa na Serikali.
“Ni muhimu kuzingatia ni kwa muda gani uwekezaji huu wa mahema utarudisha fedha za Serikali,” amesisitiza Mhe. Makoa.
Pia,
ameishukuru Serikali kwa kuwekeza fedha nyingi katika Sekta ya Utalii
kwa kuwa ni chanzo kikubwa cha mapato na kufafanua kuwa baada ya Royal
Tour ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan mabadiliko katika kuongezeka kwa mapato yatokanayo na utalii yameonekana.
Ameishukuru
pia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuendelea kuutangaza utalii
kupitia njia mbalimbali ikiwamo mikutano ya kimataifa na kuitaka Wizara
hiyo kuendelea na juhudi hizo ili iweze kuongeza tija kwa nchi.
Naye,
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameishukuru
kamati hiyo kwa kutembelea Hifadhi ya Kisiwa cha Saanane na kuahidi
kuendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha malengo ya kuongeza idadi
ya watalii yanafikiwa na mapato yatokanayo na Sekta ya Utalii
yanafikiwa.
No comments:
Post a Comment