MKUU
wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, Kanali Isack Mwakisu
amewatahadharisha wakazi wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma kuepuka
vitendo vyovyote vinavyoweza kukwamisha zoezi la anuani za makazi.
Kauli
hiyo ameitoa katika kikao kilichowahusisha viongozi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wa mkoa wa Kigoma walipokuwa wakihitimisha ziara ya siku
mbili wilayani Kasulu.
Kanali
Mwakisu ametoa kauli hiyo kufuatia baadhi ya hoja zilizowasilishwa
katika kikao hicho kuhusu migogoro ya mipaka iliyopo katika vijiji na
mitaa ya Wilaya ya Kasulu.
Amesema
kuwa, mipaka hiyo kamwe isihusishwe na anuani za makazi na
atakaposikia kuna mtu yeyote katika wilaya hiyo amesababisha kukwama
kwa zoezi la anuani za makazi, atamchukulia hatua kali ikiwa ni pamoja
na kumweka ndani.
"Rais
wetu amekwishatoa pesa nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi la
anuani za makazi, sipo tayari kusikia kuwa kuna mtu anakwamisha zoezi
hilo,"amesema.
Akizungumzia
suala la wakimbizi wanaoingia nchini bila utaratibu, amewatala wakazi
wa Wilaya ya Kasulu kushirikiana na serikali katika kukabiliana na
tatizo hilo badala ya kuitegemea Idara ya Uhamiaji na vyombo vya usalama
pekee kwa kuwa jukumu la ulinzi na usalama wa nchi ni la kila raia.
Ameongeza
pia kuwa, tatizo la wahamiaji kutoka nchi jirani ni moja ya matatizo
makubwa yaliyopo katika Wilaya ya Kasulu hivyo vyombo vya ulinzi pekee
havitaweza kutokana na ukubwa wa tatizo hilo.
Awali
katika kikao hicho, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi wa mkoa wa Kigoma
Mobutu Malima, amewaasa wataalamu na viongozi wa siasa Wilayani Kasulu
kushirikiana kwa pamoja katika kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Amesema
kuwa, kazi ya viongozi wa Chama ni kuhakikisha kuwa ilani ya Chama
inatekelezwa na kazi ya wataalamu ni kutekeleza ilani ya Chama.
Aidha,
Malima ambaye ziara hiyo ni ziara yake ya kwanza Wilayani Kasulu tangu
ateuliwe kushika wadhifa huo mwishoni mwa mwaka jana, ametoa pongezi
kwa viongozi wa Wilaya hiyo kwa kazi wanazofanya.
Kikao
hicho kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya mji wa Kasulu,
kimewakutanisha wataalamu na madiwani wa Halmashauri na mji wa Kasulu.
No comments:
Post a Comment