Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akitoa ufafanuzi kuhusu tozo ya miamala ya simu mbele ya waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es Salaam ambapo amesema wakati Serikali ikipitia upya gharama za tozo hizo, katika kipindi cha wiki nne tangu tozo hiyo ianze kukusanywa, Serikali imekusanya zaidi ya shilingi bilioni 48.4 na kuzielekeza kutekeleza miradi ya elimu, afya na miundombinu ya barabara.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu, akiwaeleza watanzania kupitia vyombo vya habari kuwa Wizara yake imepokea kiasi cha shilingi bilioni 22.5 kutoka Hazina kwa ajili ya kujenga vituo vya afya 90 kutokana na makusanyo ya tozo na kusubiri nyongeza ya shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kujenga vituo vya afya vingine 60 na kufanya idadi ya vituo hivyo vitakavyojengwa kufikia 150 katika kipindi kifupi.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Faustine Ndugulile, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kupitiwa upya gharama za tozo hizo na kuwahakikishia watanzania kuwa suala hilo linachakatwa na taarifa kamili itatolewa kwa wananchi hivi karibuni na kuwasihi waendelee kuvuta subira.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar Dkt. Juma Malik Akil, akiwaeleza waandishi wa habari kuhusu umuhimu na manufaa ya tozo ya miamala ya simu kwa maendeleo ya Zanzibar na kutoa wito kwa Wazanzibar kutulia wakati Serikali ikipitia tozo hizo baada ya kutolewa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni, mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania, Jijini Dar es Salaam.
Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akitoa ufafanuzi kuhusu tozo ya miamala ya simu mbele ya waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es Salaam ambapo amesema wakati Serikali ikipitia upya gharama za tozo hizo, katika kipindi cha wiki nne tangu tozo hiyo ianze kukusanywa, Serikali imekusanya zaidi ya shilingi bilioni 48.4 na kuzielekeza kutekeleza miradi ya elimu, afya na miundombinu ya barabara.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Faustine Ndugulile, wakiandika maswali yaliyoulizwa na wanahabari wakati Serikali ikitoa ufafanuzi kuhusu tozo ya miamala ya simu katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
*****************************
Na Rahma Taratibu, Dar es Salaam
SERIKALI imewaomba watanzania kuwa na subira wakati ikiendelea kushughulikia suala la tozo ya miamala ya simu na kutoa taarifa ya makusanyo ya fedha za tozo hizo katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita ambapo makusanyo yalikuwa zaidi ya shilingi bilioni 48.4 ambazo zimepelekwa kwenye miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu na miundombinu ya barabara.
Akitoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwingulu Lameck Nchemba alisema kati ya kiasi hicho cha fedha, shilingi bilioni 22.5 zimepelekwa TAMISEMI kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya 90, na kuahidi kupeleka kiasi kingine cha sh. bilioni 15 mwezi Agosti, 2021 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vingine 60 na kufanya idadi ya vituo vitakavyojengwa kufikia 150 nchi nzima.
Akifafanua kuhusu ujenzi wa vituo hivyo vya afya, Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Ummy Mwalimu alisema Wizara yake imepokea kiasi hicho cha shilingi bilioni 22.5 na kiasi chote cha fedha kimepelekwa kwenye Halmashauri husika na kiasi kingine cha sh. bilioni 15 zitakazotolewa mwezi Agosti ambapo fedha hizo zote zitapelekwa katika Halmashauri 82 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya 150.
Pia Wizara ya TAMISEMI inatarijia kupokea sh. bilioni 12 kutoka kwenye tozo, ambazo zitaenda kutumika kujenga vyumba vya madarasa 560 kwa ajili ya shule za sekondari ili kukabiliana na uhaba wa madarasa kutokana na sera ya elimu bila malipo, ambapo idadi ya wanafunzi inatarajia kuongezeka na kufikia wanafunzi 944,855 ambao watahitaji madarasa 10,447.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango- Zanzibar Dkt. Juma Malik Akil, alieleza kuwa kwa upande wa Zanzibar, katika kipindi cha wiki nne tangu kuanza kutozwa kwa tozo za miamala ya simu, Serikali imekusanya shilingi bilioni 1.6 ambazo zimeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo Visiwani humo.
Naye Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile, aliwahakikishia watanzania kuwa kikosi kazi kilichopewa majukumu ya kupitia upya gharama za tozo hizo kinaendelea kuchakata maagizo hayo na ndani ya mda mfupi watatoa mapitio yatakayotoa mwelekeo mpya katika hizo tozo na kuwaomba wa Tanzania kuendelea kuwa na subira na jambo hilo.
No comments:
Post a Comment