Benki
ya NBC kupitia huduma yake ya #NBCShambani inayowalenga wateja
wanaojishughulisha na kilimo imeongoza semina ya mafunzo kwa viongozi wa vyama
zaidi ya 200 vya ushirika (AMCOS) Mkoani Tabora kwa lengo la kuwapa mafunzo
mbalimbali yakiwemo umuhimu wa huduma za bima, matumizi ya fedha za
kigeni pamoja na elimu ya kuweka kumbukumbu za hesabu na matumizi
sahihi ya mapato yao ili waweze kukopesheka kwa urahisi. Hafla hiyo
ilifunguliwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tabora, Nd Bosco Ndunguru na
kuhudhuriwa na wadau mbali mbali akiwemo Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika
Mkoa wa Tabora, Nd Absalom Cheliga na wakulima wa zao la tumbaku kutoka wilaya
za Tabora Mjini, Sikonge na Uyui.
Pamoja na kuendesha mafunzo hayo Benki ya NBC kupitia Meneja wa
Wateja Wadogo, Nd Raymond Urassa walitoa zawadi ya pikipiki kwa Mwenyekiti wa
Chama Cha Msingi Solelansabo, Bi Mary James Merrick ili kumsaidia
katika shughuli za kuendesha chama na kuwatembelea wakulima. Pamoja na zawadi
ya pikipiki hiyo, Benki ya NBC pia ilitoa baiskeli tatu kwa wakulima kutoka kwa
vyama vya msingi mbali mbali kama pongezi kwa juhudi za kupata mazao mengikwa
msimu uliopita.
Akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Tabora,
Mkurugenzi wa Manispaa ya hiyo, Nd Bosco Ndunguru aliipongeza Benki ya NBC kwa
kuwawezesha na kuwapa mikopo na huduma za kibenki zenye gharama nafuu wakulima
wa zao la tumbaku ambalo kwa kiasi kikubwa linalochangia pato la
mkoa huo. Aidha alitoa rai kwa benki hiyo kuingia kwenye mazao mengine ili
kufungua fursa zaidi kwa wakulima wa mazao mengine. “Ni fursa kubwa sana kwa
mkulima mmoja mmoja na ambao wako kwenye vyama mkoani kwetu kwa Benki ya NBC
kuwa kwenye sekta ya kilimo na wakulima wanatakiwa kuichamgamki waanze
kuzalisha kibiashara.” Aliongeza Nd Bosco.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo wa Benki ya
NBC, Bw Raymond Urassa alisema kwamba Benki ya NBC kupitia NBC Shambani
imejipanga vizuri kuwahudumia wateja wake kupitia matawi yake nchi nzima
wakulima wa mazao mbali mbali yakiwemo tumbaku, kahawa, parachichi, pamba na
chai.
Akiongelea huduma za kibenki kwa mkulima mmoja mmoja, Nd Urassa
alisema kuwa mkulima anaweza kufungua akaunti bila kuwa na kianzio na kuendesha
akaunti bila kuwa na makato ya kila mwezi. “Pamoja na fursa ya akaunti za
shilingi na dola, akaunti za vyama vya msingi pia hazina makato lakini pia zina
gharama ndogo za uendeshaji kupeleka vyama vya msingi kuendesha shughuli zake
kwa gharama nafuu na kuongeza ufanisi.”
Kwa upande wake mnufaika wa zawadi ya pikipiki na Mwenyekiti wa
Chama Cha Msingi Solelansabo, Bi Mary James Merrick aliishukuru Benki ya NBC
kwa zawadi hiyo na kusema kuwa itamsaidia katika kuendesha shuguli zake za
chama kwa urahisi na ufanisi zaidi. Aidha alipongeza benki hiyo kwa kutoa
huduma zilizo bora na mikopo yenye riba nafuu inayowawezesha wakulima kutimiza
mahitaji yao ya pembejeo kwa wakati.
No comments:
Post a Comment