Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.
Katika kuelekea siku ya mtoto Afrika ambayo huadhimishwa kika tarehe 16 Juni, kila mwaka Serikali imesema bado kunachangamoto ya unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto hapa nchini ambapo takwimu zinaonyesha taarifa za vitendo hivyo zinaongezeka.
Akizungumza na wanahabari leo Juni 15 katika siku hiyo ambayo huadhimishwa kila mwaka, Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika ikiwemo Tanzania huadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema takwimu zinaonyesha vitendo hivyo bado vipo na kubainisha mikoa inayoongoza kuwa ni Tanga, Mbeya, Arusha na Mwanza.
"Takwimu za Jeshi la Polisi kwa miaka miwili mfululizo zinaonesha kuwa vitendo vya ukatili vinaendelea kuongezeka, ambapo kwa mwaka 2018 jumla ya matukio 14,491 ya ukatili dhidi ya watoto yaliripotiwa, ikilinganishwa na matukio 15,680 yaliyoripotiwa mwaka 2019 ikiwa ni ongezeko la matukio 1,189".
"Aidha, kwa mwaka 2018 aina ya matukio yaliyoongoza ni ubakaji (matukio 5,557), mimba za mwanafunzi (matukio 2,692) na ulawiti (matukio 1,159), ambapo mwaka 2019, matukio yaliyoongoza ni ubakaji (matukio 6,506), mimba za wanafunzi (2,830) na ulawiti (1,405)" amesema Waziri Ummy.
Amebainisha kuwa mikoa ya kipolisi iliyoongoza kuwa na matukio mengi zaidi ya ukatili dhidi ya watoto kwa mwaka 2018 ni Mkoa wa Tanga (1,039), Mbeya (1,001), Mwanza (809) na Arusha (792).
Wakati kwa mwaka 2019 ni Mkoa wa Tanga (matukio 1,156), Mkoa wa Kipolisi-Temeke (844), Mbeya (791) na Mwanza (758) na kubainisha kuwa vitendo hivyo kuongezeka ni matokeo ya uelewa wa Jamii katika kulipoti matukio hayo.
Aidha amebainisha kuwa Serikali imeendelea kutoa huduma za ustawi wa jamii katika mahabusu 5 za watoto za Mbeya, Kilimanjaro, Tanga, Arusha na Dar es Salaam.
"Mahabusu hizi zinatoa huduma za msingi ikiwa ni pamoja na malazi, chakula na unasihi wakati watoto hao wakiendelea kuhudhuria mashauri yao mahakamani" amesema.
Amesema kwa mwaka 2019 na 2020, watoto 138 waliwezeshwa kupata huduma hizi ikilinganishwa na watoto 354 mwaka 2018 na 2019.
Aidha ameeema katika kuimarisha huduma ya marekebisho ya tabia kwa watoto, Serikali kwa kushirikiana na Wadau inatekeleza programu ya marekebisho ya tabia kwa watoto waliopatikana na makosa katika Halmashauri mbalimbali Nchini.
"Programu hii imewezesha watoto waliopata huduma ya marekebisho ya tabia kuongezeka kutoka watoto 91 mwaka 2015/16 hadi watoto 501 Machi, 2020" amesema.
Katika kuimarisha Ulinzi wa Wanawake na Watoto katika ngazi za Mikoa na Halmashauri, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeanzisha Madawati ya Jinsia na Watoto katika vituo 427 nchi nzima.
Na kubainisha kuwa lengo la kuwezesha matukio ya ukatili wa kijinsia na watoto kuripotiwa katika vituo hivyo na kuwezesha watuhumiwa kuchukuliwa hatua za kisheria.
Ameongeza kuwa, "katika kuimarisha hayo, Mafunzo yametolewa kwa askari 490 wanaohudumu katika madawati hayo" amesema.
Sambamba na hilo, Serikali imeendelea kusimamia mfumo wa utoaji wa taarifa za vitendo vya ukatili dhidi ya watoto; ambapo kuanzia mwezi Juni 2017 hadi kufikia Machi, 2020 jumla ya watoto 167 walipata huduma katika nyumba salama 9.
Na kubainisha kuwa nyumba hizo zipo katika mikoa ya Arusha (2), Iringa (1), Kigoma (1), Mara (2), Manyara (1), Morogoro (1) na Mwanza (1).
Chimbuko la maadhimisho haya ni mauaji ya watoto takribani 2,000 yaliyofanywa na Utawala wa Makaburu katika Kitongoji cha Soweto, nchini Afrika Kusini tarehe 16 Juni, 1976.
Mauaji hayo yalitokea wakati wa maandamano ya wanafunzi waliokuwa wakipinga mfumo wa elimu ya kibaguzi nchini humo.
Mwaka 1991 viongozi wa Umoja wa Nchi za Afrika walifanya uamuzi wa kuienzi siku hiyo ikiwa ni kumbukumbu ya mauaji ya watoto hao.
Kauli mbiu ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa mwaka 2020 ni “Mifumo Rafiki ya Upatikanaji Haki ya Mtoto: Ni Msingi Imara wa Kulinda Haki Zao” Kaulimbiu hii inasisitiza kuweka mifumo madhubuti na rafiki ya kushughulikia mashauri ya upatikanaji haki kwa watoto.
No comments:
Post a Comment