Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiendesha Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 10 Juni 2020.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akicheza Wimbo wa Hamasa ya maendeleo pamoja na Wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 10 Juni 2020 kabla ya kuanza kwa Kikao hicho. PICHA NA IKULU
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Zanzibar, Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein wakati wakitoka kwenye Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 10 Juni 2020.
====== ======== ======= =========
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapenda kuujulisha umma wa wana CCM na watanzania kwamba Kamati Kuu (KK) ya Halmashauri Kuu ya Taifa (HKT) katika kikao chake cha kawaida imeketi leo Jijini Dodoma chini ya Ndg. John Pombe Joseph Magufuli Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kikao cha Kamati Kuu (KK) ya Halmashauri Kuu ya Taifa ambacho kimeketi pamoja na mambo mengine kimepokea taarifa zifuatazo; -
Mpango wa Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa imepokea na kujadili Mpango wa Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020. Kamati Kuu kwa kauli moja imeridhishwa na kiwango cha Maandalizi ya kuelekeza Uchaguzi Mkuu na kuelekeza kutolewa maramoja kwa ratiba ya Mchakato wa ndani wa uteuzi wa wana CCM wanaoomba kupewa dhamana ya uongozi katika vyombo vya Dola.
Maandalizi ya Mwelekeo wa Sera za CCM kwa Mwaka 2020 – 2030 na Ilani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.
Kamati Kuu imepokea taarifa ya Maendeleo ya Uandishi wa Mwelekeo wa Sera za CCM kwa Mwaka 2020 – 2030 na kujiridhisha kuwa kazi nzuri imefanyika mpaka ngazi ya Rasimu ya Pili. Kamati Kuu pia imepitia kwa mara ya pili Taarifa ya Uandishi wa Ilani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 na imepongeza Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa kwa kujumuisha maoni ya wadau mbalimbali na kuelekeza maandalizi ya mwisho ili Ilani hiyo iwasilishwe katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kwa uamuzi wa mwisho.
Taarifa ya Serikali juu ya Mapambano ya kuudhibiti ugonjwa wa Korona
Kamati Kuu (KK) ya Halmashauri Kuu ya Taifa (HKT) imepokea taarifa ya Serikali juu ya Mapambano dhidi ya ugonjwa wa Korona na hatua ambazo zimechukuliwa kuukabili ugonjwa huo kwa mafanikio makubwa Nchini.
Kikao cha Kamati Kuu (KK) ya Halmashauri Kuu ya Taifa baada ya Tafakuri ya kina juu ya Taarifa ya Serikali, kwa kauli moja kimempongeza Ndg. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Uongozi imara, msimamo thabiti na usioyumba katika kipindi chote cha mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Kamati Kuu na kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaendelea kutoa rai kwa umma wa watanzania kuendelea kuzingatia ushauri na maelekezo ya Serikali na wataalam wa Afya, Kumtanguliza Mungu kwa maombi na shukrani na kuendelea kuchapa kazi kwa bidii.
No comments:
Post a Comment