Na Said Mwishehe,Michuzi TV.
BALOZI Ali Karume ambaye ni mtoto wa muasisi wa nchi ya Zanzibar Sheikh Abeid Aman Karume amechukua fomu ya kuwania nafasi ya urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar huku akieleza kuwa baada ya kufanyika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25,2020 anatarajia kuwa Rais wa Nane.
Amesema iwapo atapata ridhaa ya kugombea nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM) na wananchi wakampa ridhaa kwa kumchagua kuwa Rais atahakikisha anaendeleza yale yote mazuri ambayo yamefanywa na Serikali ya Awamu ya Saba chini ya uongozi mahiri wa Rais Dk.Alli Mohamed Shein.
Akizungumza zaidi baada ya kuchukua fomu hiyo ya kuwania nafasi ya Urais, Balozi Karume alianza kwa kueleza kuwa anamshukuru Mungu kufika siku ya leo ambayo anaandika historia kubwa katika nchi kwa kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo kwa tiketi ya CCM.
"Namshukuru Dk.Shein na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar kwa kunaimini kwa kuniteua kwenye nafasi ya Waziri, kwenye nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, kwenye nafasi muhimu ya Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi ambaye Mwenyekiti wake ni yeye na sasa naomba ridhaa ya wananchi wa nchi hii, nategemea kuwa Rais wa Nane wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
"Mimi bahati nzuri nimepata fursa ya kuwa Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo , kwenye Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.Nimewahi pia kuwa Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano, na Usafirishaji na mpaka leo hii ni mimi ni Kaimu Waziri wa Biashara na Viwanda katika Serikali hii ya Mapinduzi Zanzibar.
"Nimepata fursa ya kuwa Balozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika nchi nyingi duniani ikiwemo Vatcan kwa Baba Mtakatifu, Marekani, nchi za Ulaya Magharibi na nilifikia wadhifa wa Mkuu wa Mabalozi wa Tanzania 2007 mpaka 2008,"amesema Balozi Karume.
Amefafanua zaidi iwapo atateuliwa na Chama Cha Mapinduzi(CCM) na kupata ridhaa ya wananchi wenzake anategemea kuendeleza dhamira ya mapinduzi zanzibar kwa kuulinda Muungano wetu na kulinda sera za Chama changu .
"Dk.Ally Mohamed Shein ambaye ni Rais wangu akishirikiana na Baraza la Mapinduzi amefanya kazi ya kutiliwa mfano nchini hasa hasa katika kuendeleza sera zilizoanzishwa na mwenyewe Mzee Abeid Aman Karume(Muasisi wa Taifa hili).Nia yangu ni kuendeleza yote mazuri pamoja na kuleta baadhi ya mengineyo.
"Katika afya iwe inapatikana bila malipo, elimu nayo endelee kuwa bila malipo, ugawaji wa ardhi uendelee kwa wananchi wenye uhitaji kwa ajili ya masuala ya kilimo, majenzi na kubwa zaidi kuendelea kujenga makazi bora.Nyumba ambazo zilijengwa na Mzee Karume zinahitaji ukarabati.
"Ipo kubwa ya kuleta usawa wa kijinsia , akina mama ni wazee wetu wametuzaa , wametulea, wengine ni dada zetu ,wengine ni binti zetu, wanawake tusiwatupe mbali, twende nao bega kwa bega , mkono kwa mkono katika kuijenga nchi yetu,"amesema.
Ameongeza pia atahakikisha watoto wanalindwa, wazee wanatunzwa na vijana wanapata elimu iliyo bora ambayo itawawezesha kujitegemea na kupata ajira."Ujamaa na mshikamano ndio ngao yetu.Nawaombeni nyote mniombee kwa Mwenyezi Mungu,"amesema Balozi Karume katika hotuba yake hiyo ambayo pamoja na hayo ameeleza mambo mengi kwa kina na kutoa ufafanuzi katika masuala mbalimbali.
No comments:
Post a Comment