Na Said Mwishehe,Michuzi TV
NAONDOKA Yanga!Hiyo ni kauli ya Mshambuliaji wa timu ya Yanga David Molinga 'Falcao' amesema baada ya mkataba wake ambao umbakia miezi miwili kuanzia sasa ataondoka katika kikosi hicho huku akitoa tuhuma kwa Kocha Msadizi wa timu hiyo Boniface Mkwasa kuwa hampendi.
Molinga aameeleza hayo leo Juni 10,mwaka 2020 wakati akihojiwa na watangazaji wa kipindi cha Sports Arena kinachorushwa na Wasafi FM ambapo ametumia nafasi hiyo kufafanua mambo mbalimbali yanayomhusu yeye na timu yake.
Akiwa katika kipindi hiki Molinga ameonesha kutofurahishwa na kitendo cha jina lake kutokuwemo kwenye kikosi kinachosafiri kwenda mkoani Shinyanga kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mwadui FC.
Kwa kukumbusha tu, Ligi Kuu Tanzania Bara inaanza Juni 13 mwaka huu baada ya kusimama kwa muda kutokana na janga la Corona. Hivyo mchezo wa Yanga na Mwadui ni kiporo na kikosi hicho kimeondoka leo asubuhi, ukiondoa nyota mshambualiji na kinara wa mabao katika timu hiyo Molinga
Molinga amesema yeye ni mchezaji anayejua wajibu wake na amekuwa akienda mazoezi kila siku lakini anashangaa kuona jina lake halimo kwenye orodha ya wachezaji wanaondoka na timu wakati wachezaji wengine ambao hata mazoezini hawaonekani wanasafiri na timu.
"Nilikuwepo mazoezini hadi jana jioni na jina langu halikuwemo katika orodha ya wanaosafiri na timu. Nimekuja Tanzania kwa ajili ya kucheza mpira na mimi ni profesinal,"amesema Molinga na kuongeza sio vizuri alichofanyiwa.
Alipoulizwa iwapo hana maelewano mazuri na Kocha, amejibu "Hapana hakuna shida , Kocha ndio anapanga wachezaji, ndio anachagua. Sina nachodai , niko poa, mimi ndio mfungaji bora wa timu.Mimi kama mchezaji nishacheza timu nyingi.
"Nimekuwa mfungaji bora, kila ligi mimi nacheza na nafunga si chini ya goli 18 kwa kila msimu.Kocha anatakiwa kuwa na mimi, nacheza Yanga na ndio mfungaji bora wa timu lakini bahati mbaya mambo yanakuwa kama hayo.Haiwezekani niongee kitu kibaya,niko fresh , niko pamoja na timu,"amesema Molinga.
Alipoulizwa kuwa amekuwa na changamoto ya kugoma kugoma, amesema yeye hana tatizo na mtu na wala hagomi kama inavyodaiwa lakini Kocha ndio anachagua wachezaji sio shida yake.
Kwa upande wake Msemaji wa Klabu hiyo Hassan Bumbuli amesema ni kweli kikosi kimeshaondoka leo asubuhi kikiwa fiti na wameondoka kwa basi la timu.
"Ni kweli Molinga hajasafiri na timu na Meneja alikwenda kuzungumza naye asubuhi ya leo lakini sijui kimetokea nini ila inaonekana amegoma kuondoka na timu.Hivyo tutakaa na uongozi kujua sababu za kutoondoka na timu,"amesema.
Kuhusu ushiriki wa Molinga kwenye mazoezi, Bumbuli amesema amekuwa akishiriki vizuri sana na hata jana wakati majina yanatajwa ya wachezaji wanaosafiri na timu jina lake lilikuwepo lakini ilipofika asubuhi hakuna aliyejua kama hajaripoti kambini hadi walipokuwa wanataka kuondoka ndio akapigiwa simu na akajibu yuko nyumbani.
Wakati huo huo Meneja wa Timu ya Yanga Abeid Mziba ambaye ndiye aliyemfuata Molinga nyumbani kwake kwa ajili ya kumtaka aungane na wachezaji wa kikosi hicho kuelekea Shinyanga amesema mshambuliaji huyo ana matatizo kidogo ya kufikiri kwani jana wakati Mwalimu anataja listi wachezaji wote walisikia kwanini yeye hakusikia jina lake.
"Tunaosafiri nao wote wamesikia, kwa hiyo yeye peke yake ndio hajasikia? Wakati Mwalimu anaita majina ya wachezaji, alitaja jina la mchezaji mmoja mmoja , sasa tunashangaa hadi asubuhi hajafika kuungana na timu.Nikaamua kwenda hadi nyumbani kwake na nimeingia mpaka chumbani kumbembeleza lakini amekataa.
"Nikamwambia kama hujasikia mimi ndio Meneja wa timu, twende tuungane kwenye safari tukapambane kwa ajili ya timu.Lakini akajibu mimi(Molinga) siendi kwa madai hajasikia jina lake.Nimembeleza sana na nilijusha lakini hakuwa tayari,"amesema Mziba.
Mziba alipoulizwa nini hatma ya mchezaji huyo amejibu "Tayari nimezungumza na Bumbuli ambaye tuko naye safarini, na kisha tutatoa taarifa kwa uongozi ambao utajua cha kufanya. Wakati tunaachana mazoezi hakukua na tatizo lolote Mwalimu Mkwasa aliwaita wachezaji wote na akataja listi.Wote wamekuja kasoro yeye.
"Hata katika listi yangu ya majina ya wachezaji ambayo ninayo hapa jina lake lipo na ni jina namba 17.Ila amekuwa akifanya hivyo mara kwa mara hata wakati tunakwenda Moshi aligoma hivyo hivyo. Hatuji anafikiria nini wakati hapa ni kazini kwake.Tulimuonya lakini sasa amerudia tena,"amesema Mziba.
Hata hivyo Molinga alipata nafasi tena ya kufafanua kuhusu maelezo ambayo yametolewa na Mziba ambapo amesema "Ni uongo , sio kweli kwamba nimegoma kusafiri na timu.Kilichonileta Tanzania ni mpira.This is too Much.Tangu siku ya kwanza ya mazoezi nimekuwa pale na hadi jana jina langu halikuwepo lakini jina Bernard Morrison lilikuwepo wakati hata kwenye mechi ya kirafiki hakuwepo kutokana na majeraha aliyonayo.
"Leo asubuhi ndio nafuatwa naambiwa niko safarini, mimi sio kama mtoto.Kocha ameweka list ya wachezaji na jina langu halikuwepo. Nimegoma kwasababu mimi ni mfungaji bora wa timu, sio mchezaji mdogo katika timu, kwanini Kocha anaweka list ambayo kuna wachezaji wengine hawakufanya mazoezi , kocha anazungumza mambo ya fitness wakati watu wako nyumbani.
"Kocha anapanga timu kulikanga na mazoezi lakini Kocha anapanga kulingana na mtazamo wake.Nataka kusema ukweli leo Yanga wanisikie ...Mkwasa hanipendi mimi, niko hapa kwa ajili ya mpira na sio kwasababu ya mtu fulani,"amesema Molinga.
Ameongeza kuwa mkataba wake unaenda mwishoni kwani amebakisha miezi miwili na hivyo baada hapo ataondoka , hawezi kuendelea na kuwa kwenye kikosi hicho.
Kuhusu kilo zake, Molinga amesema kwa sasa ana kilo 88 kutoka kilo 85 kabla ya Corona lakini ukweli ni kwamba wakati anakuja Tanzania alikuwa na kilo nyingi lakini kwa kuwa anajua wajibu wake amejikondesha sana.
"Hizo kilo tatu zinatokana na kufanya mazoezi ya kufanya mwenyewe, ambayo ni tofauti na kuwa na mazoezi ya pamoja.Wakati nakuja hapa nilikuwa na kilo nyingi sana, na sasa nimekonda sana lakini sasa nachafuliwa.Msemaji wa klabu anakwenda mitandaoni badala ya kuniuliza mimi moja kwa moja,"amesema Molinga.
No comments:
Post a Comment