Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza Vyuo vyote vifunguliwe rasmi kuanzia Tarehe 01.06.2020 kutokana na kupungua kwa kiasi kikubwa Maambukizi ya Virusi vya Corona (COVID-19).
Rais Magufuli amesema hayo leo Alhamis Mei 21,2020 Ikulu Chamwino Dodoma wakati akiwaapisha viongozi aliowateua.
Pia amesema Vijana wanaosoma Form Six/Kidato cha Sita waliokuwa wanajiandaa kufanya mtihani wao wa Kumaliza Elimu ya kidato cha sita waanze masomo tarehe 01.06.2020
Kuhusu Shule za Msingi na Sekondari, Rais Magufuli ameagiza Shule hizo kujipa muda kidogo kuangalia hali ya Maambukizi ikoje katika kipindi hiki maambukizi hayo yanaendelea kupungua zaidi.
"Wanafunzi Shule za Sekondari na Msingi tuzipe muda kidogo, hawa Wakubwa Vyuoni wanajitambua, wanaelewa zaidi kuhusu masuala ya Maambukizi, sisi wa huku tujipe muda kidogo", amesema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli ameagiza Michezo yote zikiwemo Ligi nazo zifunguliwe Juni 1,2020.
“Katika trend tuliyoiona sina uhakika kama kuna mwanamichezo aliyekufa kwa corona na michezo ipo mingi kila mmoja ana michezo yake, lakini michezo inasaidia kupambana, kwa hiyo kuanzia June 01,2020 michezo irudi kama kawaida, ligi mbalimbali”, amesema.
“Kuanzia June 01,2020, michezo ianze, kuanzia ligi hiyo iliyokuwepo, ligi daraja la kwanza, la pili, n.k iendelee, taratibu za kushangilia na kuangalia Wizara ya Afya na inayohusika na Michezo watapanga ili utaratibu wa social distance ukaendelea kuwepo”,amesema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli ameagiza Mamlaka zinazohusika na masuala ya Utalii kuhakikisha wanasimamia ipasavyo ujio wa Watalii hapa nchini ifikapo Mei 27-28, 2020 sambamba na kuruhusu Ndege za Watalii hao kutua nchini. "Wakitaka kuja kujifukiza na Nyungu waje tu", ameeleza Rais Magufuli.
Rais Magufuli ameagiza Wizara ya Elimu na Fedha kuhakikisha Wanafunzi hao wa Vyuo wanaorejea Vyuoni humo wanapatiwa Mikopo yao kwa muda mchache uliobaki.
Pia Rais Magufuli ameagiza Wizara ya Afya kuratibu utaratibu maalum kwa Wanamichezo inaporejea June 1 ili kuhakikisha tahadhari inaendelea kuchukuliwa dhidi ya Maambuzi ya Virusi vya Corona ambavyo vimepungua kwa kiasi kikubwa hapa nchini
No comments:
Post a Comment