YANGA imefanya maamuzi magumu kwa kuwapukutisha mastaa watano wa kigeni akiwemo Sadney Urikhob ambae amewawahi kwa kuandika barua ya kuvunja mkataba. Jumamosi iliyopita kwenye mitandao ya kijamii zilisambaa habari za wachezaji kadhaa wa Yanga kuvunja mikataba kwa madai kwamba hawajalipwa mishahara kwa miezi mitatu.
Habari za uhakika ambazo Spoti Xtra imezipata ndani ya Yanga jana ni kwamba wachezaji hao wanadai mishahara ya Oktoba na Novemba lakini jana viongozi walikuwa wanakwepa kutoa ufafanuzi rasmi licha ya presha ya mitandaoni.
Chanzo makini ndani ya uongozi kimelithibitishia Spoti Xtra kwamba wamepanga kuachana na wachezaji watano wa kigeni ambao wamekuwa ni mizigo kwa klabu. “Mishahara siyo miezi mitatu, ni kweli wanadai lakini ni Oktoba na Novemba tu, Desemba si ndio kwanza imeanza? Utauhesabiaje?” alihoji kiongozi huyo na kuongeza.
“Hizi vurugu za wachezaji kuna baadhi ya watu wanaichochea kwa makusudi kabisa lakini sisi tayari tulishajua nani tunamuacha na karibu wote wanajua, hao wanaozungumza mitandaoni wote wanajua wanaachwa na barua zao wanazo.”
Kiongozi huyo alisema kwamba Yanga imepanga kuwatema wachezaji watano wa kigeni ambao wameona hawana faida nao kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao ndani ya uwanja kwa mujibu wa mikataba.
Aliwataja wachezaji wanaobaki kuwa ni David Molinga, Patrick Sibomana, Lamine Moro, Papy Tshishimbi na Farouk Shikhalo. Wanaotemwa kutokana na majeruhi na viwango ni Sadney Urikhob, Juma Balinya, Maybin Kalengo, Issa Bigirimana na Mustafa Suleiman.
“Mtu kama Kalengo na Bigirimana tumeshawaambia muda mrefu kwamba hatutakuwa nao kutokana na hali zao na viwango vyao, huyo Sadney na yeye pia tulishamwambia alichofanya ni kukimbilia kwenye mitandao kujikosha kwa vile aliona akitangazwa atadhalilika.
“Hao wengine ishu za mishahara tutamalizana nao tu kwa vile kuna mambo mengi tulikuwa tunayaweka sawa, safari hii tutasafisha sana timu usajili mkubwa wa Zahera (Mwinyi) utaondoka,” alisisitiza kiongozi huyo.
Habari zinasema kwamba Yanga waliisuka mikataba ya wachezaji wengi kiakili ili wasije kulipa fidia kubwa na wachezaji wengi wanaoondoka wamenasa kwenye kifungu cha uwajibikaji.
Licha ya kwamba baadhi ya viongozi wanadaiwa kuwa upande wa wachezaji hao wanaoshinikiza kulipwa stahiki zao, habari zinasema kwamba hata kwenye wachezaji wa ndani litapita panga ambao watano au sita watapelekwa kwa mkopo kwenye timu zingine ikiwemo Singida United.
Miongoni mwao ni beki mfupi, Mwarami Isa ‘Marcelo’ na Ally Ally. Dirisha dogo la usajili wa Ligi Kuu Bara linafunguliwa Desemba 16 na kufungwa Januari 15, mwakani.
No comments:
Post a Comment