Waziri wa Kilimo
nchini Tanzania, Japhet Hasunga leo Septemba 2, 2019 ameshiriki mahafali ya mafunzo
ya Kilimo ya Agro Studies yaliyofanyika mjini Jerusalem nchini Israel na
kuwatunuku vyeti vya kuhitimu wanafunzi 45 kutoka Tanzania.
Katika ukumbi wa kimataifa wa
mikutano wa ICC (Jerusalem International Conventional Center), Waziri Hasunga
amewapongeza vijana hao kwa kuhitimu masomo yao hivyo amewaahidi kuwa serikali
ya Tanzania inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli imejipanga kuboresha
mazingira wezeshi kwenye sekta ya kilimo hivyo wanayo nafasi nzuri kuutumia
ujuzi walioupata kuboresha kilimo watakaporejea nchini Tanzania.
Mahafali hayo yamejumuisha vijana
1600 kutoka mataifa zaidi ya 12 ambapo kati ya hao vijana 45 ni watanzania,
miongoni mwao wanawake wakiwa ni 9 na wanaume ni 36.
Waziri huyo wa kilimo wa Tanzania,
Japhet Hasunga amesema kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepewa
jumla ya nafasi 100 kwa ajili ya kupeleka vijana wa kitanzania kujifunza kilimo
cha kisasa nchini Israel hivyo fursa hiyo ni muhimu kwani vijana wa Tanzania watapata ujuzi kwa manufaa makubwa
nchini mwao.
Akizungumza mara baada ya
kuwakabidhi vyeti wahitimu hao Mhe Hasunga amesema kuwa kupatikana kwa nafasi
hizo 100 ni kutokana na ombi la Rais wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli kwa serikali ya Israel ili
kuwawezesha vijana wengi wa kitanzania kujifunza mbinu na teknolojia za kilimo
cha kisasa.
Kadhalika, Waziri Hasunga amekutana
na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Agro Studies ambapo miongoni mwa mazungumzo
muhimu aliyoongea nae ni pamoja na kumuomba uwezekano wa kuongezewa nafasi
zaidi ili vijana wengi wa kitanzania waende kujifunza mbinu mpya za kilimo
nchini Israel.
Pia, Mhe Hasunga alifanikiwa kukutana
na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo nchini Israel kujadiliana nae maeneo
mbalimbali na fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya kilimo nchini
Tanzania.
Katika mkutano mwingine, Mhe
Hasunga atakutana na kufanya mazungumzo na wadau wawekezaji wakubwa wa sekta ya
kilimo nchini Israel ili kuwaeleza fursa za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania.
No comments:
Post a Comment