Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamini Mkapa mara baada ya kuhutubia katika wa mkutano wa wa 39 wa Wakuu wa nchi na Serikali za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Rais Mstaafu wa Awamu ya nne Jakaya Mrisho Kikwete na kulia ni Rais Mstaafu wa awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi . PICHA NA IKULU
Kongo yashauri kuundwa na kundi la kikanda kukomesha uovu
Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
MWENYEKITI aliyemaliza muda wake katika Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambaye ni Rais wa Namibia Dkt. Hage Geingob amesema Tanzania ni mfano wa kuigwa kutokana ushirikiano na umoja wa viongozi wao.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika ufunguzi rasmi wa mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi na serikali uliofanyika leo katika kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam ,Dkt.Hage amesema;
"Tanzania ni mfano wa kuigwa, ona marais wastaafu wamekaa pamoja na wameonesha ushirikiano mkubwa kwetu na hata mawaziri wastaafu wapo hapa, namwona John Malechela na wengine wengi kweli mnastahili pongezi" ameeleza Hage.
Aidha amempongeza Rais wa Kongo Felix Tshesekedi kwa kufanikisha kubadilishana madaraka kwa usalama nchini humo na kushauri kwa nchi jumuiya lazima zijikite katika kulinda amani na uhimilivu kama msingi mkuu wa maendeleo.
Kuhusu mabadiliko ya tabia nchi ndani ya ukanda huo Dkt.Hage amesema kuwa majanga ya mafuriko na vimbunga yamezikumba baadhi ya nchi za jumuiya hiyo zikiwemo Malawi na Msumbiji ambapo zaidi ya watu 3000 waliathirika.
"Shukrani za dhati ziende kwa nchi wanachama kwa kutoa msaada wa haraka kwa nchi zilizoathirika na majanga hayo na ninashauri tuchukue tahadhari za haraka ikiwa ni pamoja kuwashauri wananchi kupanda na kutokata miti na kutoa taarifa za haraka kwa wananchi kuhusiana mabadiliko ya tabia nchi," ameeleza.
Pia amewahimiza nchi za Jumuiya kuwekeza zaidi katika kundi la vijana ili kuweza kupata maendeleo endelevu ili kufikia malengo ya mwaka 2025 waliyojiwekea kupitia programu mbalimbali zikiwemo za nishati, maji na miundombinu katika ngazi mbalimbali za kitaifa na kimataifa na hiyo ni pamoja na kuwa na kuangalia tafiti na gunduzi ili kuweza kuinua kundi hilo la vijana kupitia sera madhubuti.
Alisema robo tatu ya wananchi wa Jumuiya hiyo ni vijana,hivyo wakitumika vizuri katika kuleta maendeleo nchi zetu zitapiga hatua kiuchumi.
Awali akihutubia katika mkutano huo Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshesekedi amezishukuru nchi wanachama ikiwemo Tanzania kwa mchango wao wakati wa kubadilishana madaraka kwa amani zaidi na kwa sasa hali ya amani Kongo inazidi kuimarika licha ya eneo la Mashariki mwa nchi hiyo bado kunatishiwa na kundi la kigaidi ambalo ni tishio kubwa ila wametengeneza mkakati wa kuimarisha mamlaka ya serikali ili kuimarisha amani.
Aidha Tshesekedi ameziomba nchi wanachama kuimarisha umoja na mshikamano na kushauri kuwa mwisho wa mkutano huo watoke na tamko la kuwa na kundi la kikanda la kukomesha uovu ili kuzidi kuimarisha nchi wanachama kiusalama na uchumi.
Kuhusiana na kauli mbiu ya mkutano huo wa 39 inayosema "Mazingira wezeshi kwa maendeleo endelevu na Jumuishi ya Viwanda, kuongeza Biashara na Ajira Kikanda" Tshesekedi amesema kuwa jumuiya ya Kongo ina mipaka na nchi nyingi na fursa nyingi hupatikana kupitia mabwawa ya nishati na amehahidi ushirikiano na na kushauri kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara ili wananchi waweze kufanya biashara na kujenga uchumi wa jumuiya kwa ujumla.
Pia ameshauri nchi wanachama kuzingatia kilimo pamoja na ujenzi wa mabwawa ya kuzalisha umeme ili kuweza kufikia azma ya kufanya mapinduzi ya viwanda na anaamini mkutano huo utafikia malengo makubwa ndani ya jumuiya hiyo.
Tshesekedi amepongeza mwenyekiti anayemaliza muda wake na kueleza kuwa Hana mashaka na mwenyekiti mpya Rais Magufuli na agenda yake wa kujenga Viwanda katika ukanda huo wa SADC wanaamini itafikiwa vyema na kumalizia kwa kusema kuwa lazima jumuiya ijipongeze kwa kukichagua Kiswahili kuwa lugha rasmi ya jumuiya hiyo.
Marais wastaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Dkt. Jakaya Kikwete, Mh. Benjamin Mkapa pamoja na Mh Ally Hassan Mwinyi wakifuatilia yanayojiri kwenye mkutano wa 39 wa SADC uliofanyika leo katika kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam .Picha Michuzi JR
No comments:
Post a Comment