A great place to access the latest news and information.

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Friday, March 22, 2019

Maafisa Habari wa Serikali wasisitizwa kutangaza jambo hili


Maafisa Habari wa Serikali wamesisitizwa kuendelea kutangaza mageuzi makubwa yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Hayo yamesemwa leo Jijini Mwanza na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza alipokuwa akifunga Kikao Kazi cha 15 cha Maafisa Habari wa Serikali kilichofanyika jijini humo kwa siku tano.

Bi Shonza amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imefanya mageuzi makubwa tangu iingie madarakani mwezi Novemba mwaka 2015 ambapo wananchi wameshuhudia mageuzi mbalimbali katika Sekta za Afya, Elimu, Maji, Usafiri wa Anga, Miundombinu ya Barabara, Reli na viwanja vya ndege.

“Mafanikio yote haya yanapaswa kuelezwa kwa wananchi, jukumu hilo ni la nyinyi Maafisa Habari wa Serikali hivyo ni imani yangu kuwa mafunzo na uzoefu mlioupata kupitia Kikao Kazi hiki yataleta chachu ya kutangaza zaidi shughuli za Serikali kupitia njia mbalimbali zikiwemo Televisheni, Magazeti, Tovuti pamoja na mitandao ya kijamii”, alisisitiza Bi Shonza.

Akifafanua kuhusu maagizo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yaliyotolewa wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Naibu Waziri Shonza amesema kuwa maelekezo yaliyotolewa kwa viongozi wa Serikali na Maafisa Habari wa Serikali yamelenga katika kuboresha Sekta hiyo na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati juu ya utekelezaji wa Serikali hivyo ni lazima yazingatiwe na kutekelezwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa kikao hicho kimehudhuriwa na takribani Maafisa Habari wa Serikali 400 ambao wamepata mafunzo kupitia mada mbalimbali zilizotolewa ambazo zimejikita katika kuboresha utekelezaji wa kada ya habari.

“Kwa umoja wetu tumepata wasaa wa kutathmini na kuchambua mambo mbalimbali tunayopaswa kufanya na yale ambayo Serikali inatakiwa kufanya pia kwa kuwa hakuna muongozo wa matumizi ya mitandao ya kijamii, kupitia kikao kazi hiki tumejadili na kupata rasimu ambayo tutaiboresha na hivi karibuni Kada ya Habari itakua na muongozo wa kutumia mitandao ya kijamii”, alisema Dkt. Abbasi.

Miongoni mwa mambo yaiyojadiliwa ni pamoja na mbinu za medani za kihabari wakati wa dharura, Mwongozo wa maudhui mitandaoni, Mbinu na mkakati wa kuboresha uhusiano na vyombo vya habari, Usanifu wa lugha na uandishi mzuri wa taarifa kwa umma, Mbinu aushi za upigaji picha jongefu za habari na makala pamoja na habari za uongo katika kazi za Maafisa Habari na Mikakati ya Kukabiliana nazo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages