UONGOZI wa Klabu ya Yanga umeweka bayana kuwa utamalizana na wachezaji wake juu ya malimbikizo ya fedha zao muda mfupi baada ya kurejea kutoka nchini Algeria ambako kikosi hicho kilienda kwa ajili ya kucheza mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga jana Jumapili ilikuwa nchini Algeria kwa ajili ya mchezo wake huo wa Kombe la Shirikisho Afrika kupambana na wenyeji wao USM Alger ambapo kikosi hicho kiliwakosa nyota wake saba wa kikosi cha kwanza kutokana na matatizo mbalimbali huku ikitajwa wengine waligomea safari hiyo kutokana na kudai fedha zao.
Wachezaji ambao hawakusafiri na timu hiyo ni pamoja na Obrey Chirwa, Papy Tshishimbi, Ibrahim Ajibu, Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Donald Ngoma na Thaban Kamusoko.
Akizungumzia juu ya hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika, alisema kuwa wanatambua nyota wao wanaidai fedha klabu yao lakini wanapambana kuhakikisha wanamalizana nao muda mfupi baada ya kikosi hicho kurejea kutokea nchini Algeria.
“Tunajua kwamba wachezaji wetu wanadai fedha zao lakini kama uongozi tunapanga namna ya kumalizana nao kwa ajili ya kuwapa stahiki zao, na tumepanga muda mfupi baada ya kurejea nchini tukitoka Algeria basi tuwalipe kile ambacho wanatakiwa kupewa.
“Kama uongozi tunapambana kwa kila namna kuona tunawapa fedha zao japo ilitakiwa wachezaji wapambane kuona timu inafika hatua za mbali katika kombe hili kwa ajili ya kuingiza fedha nyingi zaidi ambazo zitarahisisha wao kupata malipo mazuri zaidi,” alisema mwenyekiti huyo.
No comments:
Post a Comment