SIKU chache baada ya beki wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani, kumtemea mate beki wa Simba, Asante Kwasi na suala hilo kupelekwa katika Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho ya Soka Tanzania (TFF), hofu kubwa imezuka makao makuu ya klabu hiyo.
Yondani alimtemea mate Kwasi hivi karibuni katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliozikutanisha Yanga na Simba katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wapenzi na mashabiki wa timu hiyo, wamejawa na hofu ya kumkosa mchezaji huyo katika mechi zao zote za ligi kuu zilizobakia, jambo ambalo wanaamini kuwa linaweza kusababisha wakamaliza ligi hiyo wakiwa katika nafasi ya tatu ambayo wanashika sasa wakiwa na pointi 48, nyuma ya Azam yenye pointi 49, pamoja na Simba ambayo kabla ya mechi yake ya jana ilikuwa na pointi 62.
Jana, Jumapili Championi Jumatatu lilizungumza na baadhi ya mashabiki wa Yanga makao makuu ya klabu hiyo kuhusiana na suala hilo la Yondani na baadhi yao walionyesha hofu hiyo.
“Tunasubiri tuone ni adhabu gani atakayopewa lakini hofu yetu tuliyonayo sasa ni kwamba tunaweza kumkosa katika mechi zetu zote zilizobakia na ukizingatia ni mchezaji muhimu sana katika kikosi chetu msimu huu,” alisema mmoja wa mashabiki hao ambaye alijitambulisha kwa jina la Salum Juma.
Shabiki mwingine wa timu hiyo ambaye alijitambulisha kwa jina na Emmanuel Temba, alisema: “TFF inatakiwa kutenda haki katika hilo, kama ni adhabu basi aadhibiwe kwa mujibu wa kanuni lakini siyo kwa ajili ya kutaka kumkomoa kutokana na mashinikizo ya baadhi ya watu wasiotutakia mema.
“Bado tunamhitaji sana Yondani katika mechi zetu za ligi zilizobakia lakini pia katika michuano ya kimataifa, kwa hiyo wasitoe adhabu ambayo inaweza kusababisha asionekane tena uwanjani mpaka mwisho wa ligi.”
Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni ya 37 ya ligi kuu inayozungumzia udhibiti wa wachezaji, adhabu kubwa ambayo Yondani anaweza kukumbana nayo kutokana na kosa hilo ni kifungo cha mechi tatu pamoja na kulipa faini ya Sh 500,000.
No comments:
Post a Comment