KIUNGO mchezeshaji wa Simba, Haruna Niyonzima, raia wa Rwanda, ameibuka na kuweka wazi kuwa anachekelea kwa kuwa anaweza kuweka rekodi ya aina yake, ya kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo akiwa na timu mbili tofauti za Yanga na Simba.
Niyonzima aliyetua Simba mwanzoni mwa msimu huu, msimu uliopita wakati akiwa Yanga alifanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi kwa kuwazidi Simba kwa idadi ya mabao ya kufunga ambapo pia msimu huu yupo kwenye nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kwa mara nyingine kutokana na timu yake hadi sasa kuwa kileleni mwa msimamo.
Hadi jana Jumapili Simba ndiyo walikuwa wanaongoza ligi wakiwa na pointi 62 (kabla ya mechi yao na Ndanda FC), pointi ambazo zinawaweka mbele kwa tofauti ya alama 14 dhidi ya wapinzani wao Yanga ambao wanakamata nafasi ya tatu.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mnyarwanda huyo alisema kuwa kwake anafurahia kwa kuwa anakaribia kuweka rekodi hiyo kwa upande wake ambapo inakuja baada ya wao kuweka mipango ya kutwaa taji tangu wanaanza ligi.
“Kama nilivyosema awali kwamba Simba kwa sasa hatuna cha kupoteza kwenye mechi zetu, tutapambana kuona kwamba tunapata pointi katika kila mchezo ambao tutashuka dimbani kuona tunalikamilisha suala la kutwaa ubingwa.
“Lakini kwangu kama nitafanikiwa kuweka rekodi hiyo basi nitajisikia mwenye furaha kwa sababu nitafanikisha kile ambacho tulikipanga na jambo hilo naweza kulisema kwamba kama neema kwa upande wangu,” alisema Niyonzima.
No comments:
Post a Comment