YANGA usiku wa kuamkia leo ilicheza mechi yake ya kwanza ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika bila ya nyota wake saba waliojiondoa kikosini kwa sababu mbalimbali.
Licha ya kila mchezaji kati ya hao saba kuwa na sababu ya kutokuwepo kikosini, taarifa zinasema wachezaji hao hawapo kikosini wakishinikiza walipwe mishahara yao ya miezi ya nyuma.
Wachezaji hao saba ni mbali ya Amissi Tambwe na Donald Ngoma ambao ni majeruhi wa muda mrefu katika kikosi cha timu hiyo kongwe nchini ikiwa imeanzishwa katika miaka ya 1930.
Yanga imecheza na USM Alger bila ya nyota hao ambao kwa hakika wangeongeza kitu katika mchezo huo wa Kombe la Shirikisho.
Suala la kudai kwa wachezaji wa Yanga halikuanza ghafla, bali ni kitu cha muda mrefu ambacho kingeweza kutatuliwa ama kwa kuwaeleza ukweli wachezaji au kuita wadau wengine ili wasaidie.
Uongozi wa Yanga ungezungumza wazi kwamba hauna fedha za kuwalipa wachezaji hao kwa sasa na hata wachezaji wangejua lakini ahadi isiyotekelezeka imekuwa fimbo ya mgomo baridi huu wa sasa.
Wachezaji hawa nao ni binadamu wanaotegemewa na familia zao ambao soka ndiyo kila kitu kwao, sasa wasipopata mshahara inaweza kuwa kikwazo cha kuendesha maisha yao.
Yanga ina wanachama wengi wenye fedha zao lakini kama uongozi unakaa kimya bila ya kuwafuata na kuwaeleza ukweli kuhusu nafasi ya klabu kiuchumi kamwe hawawezi kutoa chochote.
Kila mahali hali ya kifedha ni mbaya, hivyo ni jukumu la Yanga kuwa wakweli ili waweze kupata msaada na hili ni somo kwa timu nyingine ambazo hazipendi kueleza ukweli wa mambo katika timu zao.
No comments:
Post a Comment