Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dodoma, jana ilimpandisha
kizimbani aliyekuwa Mkurugenzi wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao
Makuu (CDA) Paschal Muragili kwa madai ya matumizi mabaya ya madaraka.
Muragili
alikuwa Mkurugenzi wa CDA hadi Mei mwaka jana ambapo Rais John Magufuli
aliamua kuivunja mamlaka hiyo na shughuli zake kurudishwa Manispaa
ambayo kwa sasa ni Jiji.
Kamanda
wa Takukuru Mkoa wa Dodoma Sosthenes Kibwengu amesema Muragili
anatuhumiwa kwa makosa ya matumizi mabaya ya mamlaka, kinyume na kifungu
cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa cha mwaka 2007.
Mbali na
mkurugenzi huyo wa zamani,Takukuru imempeleka pia aliyekuwa fundi sanifu
Lemanya Benjamini ambao kwa pamoja walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi
Mfawidhi, Emanuel Fovo wa mahakama ya Hakimu Mkazi.
Akisoma
hati ya mashtaka, Mwendesha mashtaka wa Takukuru Biswalo Biswalo
ameieleza mahakama kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo Septemba, 2016.
Hakimu
Fovo alitoa dhamana kwa washtakiwa wote baada ya kutimiza masharti ya
dhamana ambayo ni pamoja na kila mtu kuweka fedha taslimu Sh 23 milioni
au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Nyingine
ni kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika pamoja na kuwasilisha hati zao
za kusafiria na kuwa washtakiwa hao hawaruhusiwi kusafiri nje ya nchi
bila kibali cha Mahakama. Kesi itaskilizwa tena Juni 4 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment