A great place to access the latest news and information.

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Sunday, May 13, 2018

Kigwangalla afanya uteuzi huu


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kingwangalla amemteua mshindi wa taji la Miss Journalism Tanzania 2018, Witness Teddy Kavumo kuwa balozi wa utalii wa Pori la Akiba Selous.

Dkt. Kigwangalla amefanya uteuzi huo mwishoni mwa wiki Jijini Dodoma baada ya mazungumzo na mwanamitindo huyo aliyemtembelea ofisini kwake kwa ajili ya kuomba ufadhili wa kuandaa mradi wa kijamii ambao ni sehemu ya shindano atakaloshiriki la taji la Dunia la Miss Journalism 2018 litakalofanyika Oktoba 27 Jijini Arusha.

Kufuatia uteuzi huo, Dkt. Kigwangalla amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania, Devotha Mdachi kuandika barua ya uteuzi kwa balozi huyo mpya sambamba na kumkabidhi hati ya uteuzi ili pamoja na mambo mengine aweze kunadi vivutio vya utalii vya pori hilo.

Wakati huo huo, Dkt. Kigwangalla amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, Dkt. James Wakibara kuandaa safari maalum ya balozi huyo mteule aweze kutembelea Pori la Akiba Selous kwa ajili ya kuona na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu hifadhi hiyo kwa ajili ya utangazaji.

Awali akiwasilisha ombi lake kwa Waziri Kigwangalla la ufadhili wa safari yake ya ushiriki wa mashindano hayo, Witness pia aliomba kupewa fursa ya kuwa balozi wa Tanzania kwenye moja ya sekta ikiwemo Misitu, Nyuki au Utalii.

Mbali na kushikilia taji la Miss Journalism Tanzania 2018, Witness amesema amewahi kushinda mataji mengine manne makubwa ya kimataifa ya ulimbwende nchini Afrika ya Kusini anakosomea urubani kwa sasa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages