Serikali ya Uganda imewasafirisha kwa usafiri wa anga walionusurika katika ajali mbaya iliyotokea katika wilaya ya Kiryandongo Ijumaa usiku nchini humo.
Gazeti la Daily Monitor nchini Uganda limeripoti kuwa basi linalomilikiwa na kampuni ya Gaagaa bus ambalo lilikuwa safarini kutoka wilaya ya Lira liligonga trekta ambayo ilikuwa inaelekea kitongoji cha Karuma wilaya ya Kiryandongo.
Polisi wamesema basi hilo liligonga trekta kwa nyuma na baada ya hapo, kupoteza muelekeo na kusababisha kugongana uso kwa uso na gari la mizigo lililokuwa limebeba kreti za bia, ambalo lilikuwa linatokea Kampala.
“Watu 19 walipoteza maisha papo hapo wakiwemo madereva watatu. Watu wengine 25 walikimbizwa hospitali na kulazwa katika hospitali ya Kiryandongo,” msemaji wa Polisi wa mkoa wa Albertine Julius Hakiza amesema.
Uongozi wa hospitali ya Kiryandongo umesema kuwa mpaka Jumamosi asubuhi, walikuwa tayari wamepokea miili 23 katika sehemu ya kuhifadhia maiti.
Eneo la ajali lilikuwa limetapakaa damu, vipande vya nyama ya binadamu, na vipande vya chupa vinavyotokana na vio vya mbele ya gari.
No comments:
Post a Comment