Duniani
kote, vifo vya watoto wachanga bado viko juu sana kiasi cha kuwa
tishio, hasa miongoni mwa nchi maskini zaidi ulimwenguni, UNICEF imesema
katika ripoti yake mpya kuhusu vifo vya watoto iliyozinduliwa leo mjini
New York. Ripoti hiyo imebainisha kuwa watoto wanaozaliwa katika nchi
za Japani, Iceland na Singapore wana nafasi kubwa zaidi ya kuishi,
wakati wale wanaozaliwa katika nchi za Pakistani, Jamhuri ya Afrika ya
Kati na Afghanistani wanakabiliana na hatma mbaya kabisa ya maisha yao.
“Wakati
ambapo tumepunguza kwa zaidi ya nusu idadi ya vifo miongoni mwa watoto
wenye umri wa chini ya miaka mitano katika robo karne iliyopita, bado
hatujafaulu kwa kiwango kama hicho katika kukomesha vifo miongoni mwa
watoto walio na umri wa chini ya mwezi mmoja,” alisema Henrietta H.
Fore, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF.
“Kwa
kuwa vifo hivi vingi vinazuilika, ni wazi kwamba, tumewaangusha watoto
walio maskini zaidi duniani,” alisisitiza mkurugenzi huyo wa UNICEF.
Ulimwenguni, katika nchi za kipato cha chini, wastani wa vifo vya watoto
wachanga ni vifo 27 katika kila vizazi hai 1,000, ripoti inasema.
Katika nchi za kipato cha juu, kiwango ni vifo 3 kwa kila vizazi hai
1,000. Nchini Tanzania, viwango vya vifo vya watoto wachanga ni 25
katika kila vizazi hai 1,000, kwa mujibu wa Utafiti wa Demografia na
Afya wa Tanzania (TDHS 2015-16).
Ikiwa
kila nchi itapunguza viwango vya vifo vya watoto wake wachanga hadi
katika viwango vya nchi za kipato cha juu ifikapo mwaka 2030, maisha ya
watoto milioni 16 yataokolewa, ripoti hiyo imebainisha. Ripoti hiyo
inaeleza pia kwamba miongoni mwa maeneo 8 kati ya 10 yaliyo hatari zaidi
kwa mtu kuzaliwa, basi Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara, ni mojawapo,
ambapo wanawake wajawazito wana uwezekano mdogo wa kupata msaada wakati
wa kujifungua kwa sababu ya umaskini, migogoro na taasisi zisizo na
ufanisi. Watoto wanaozaliwa katika nchi zenye hatari zaidi wana
uwezekano wa hadi mara 50 wa kufa kulinganisha na wale wanaozaliwa
katika nchi zilizo salama.
Nchini
Tanzania, kuna hatua kubwa imepigwa katika kupunguza vifo miongoni mwa
watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, hata hivyo hatua hiyo bado
haijafikiwa katika kukomesha vifo vya watoto wachanga na akina mama.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye viwango vya juu sana vya vifo vya
watoto wachanga duniani: takribani watoto 39,000 hufariki kila mwaka,
miongoni mwao, 17,000 hufa katika siku yao ya kwanza duniani. Wengine
zaidi 47,550 wanazaliwa wakiwa wameshakufa na akina mama wapatao 8,000
hufa kila mwaka wakati wa kujifungua. Kuna hatua kubwa imepigwa nchini
inayowapa watoto wa Kitanzania nafasi kubwa zaidi ya kuishi hata baada
ya kutimiza miaka mitano tangu kuzaliwa kwao.
Hata
hivyo, bado kuna changamoto. Kila siku, watoto 270 wenye umri wa chini
ya miaka mitano hufa, wengi kutokana na magonjwa yanayozuilika kama vile
malaria, homa ya mapafu na kuhara. “Karibu vifo 6 katika 10 hutokea
katika siku yao ya kwanza ya maisha, wakati vifo 4 katika 10 hutokea
katika mwezi wa kwanza wa maisha. Tunaweza kuokoa vifo hivi kwa huduma
rahisi na nafuu, zilizo bora ambazo zinapaswa kumfikia na kufikiwa na
kila mama na mtoto wake mchanga kote nchini.
UNICEF
imedhamiria kuunga mkono juhudi za serikali katika kupunguza viwango
vya vifo vya watoto wachanga. Sote tunapaswa kudhamiria kumpa kila mtoto
nafasi stahiki ya kuanza maisha. Ni haki na jambo la maana la kufanya,”
alisema Maniza Zaman, Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania. Kwa mujibu
wa ripoti hiyo, zaidi ya asilimia 80 ya vifo vya watoto wachanga
vinatokana na kuzaliwa njiti, matatizo wakati wa kujifungua au
maambukizi kama vile homa ya mapafu na bakteria katika tishu.
Vifo
hivi vinaweza kuzuiwa kama huduma ya zuazi itatolewa na wakunga wenye
mafunzo, huku kukiwa na uhakika wa maji salama, dawa za kuzuia vijidudu,
unyonyeshaji katika saa ya kwanza, kumkumbatia mtoto na lishe bora.
Hata hivyo, upungufu wa watumishi wa afya wenye mafunzo bora na wakunga
kunamaanisha kwamba maelfu hawapati msaada huu muhimu wa kuokoa maisha
yao katika kipindi hiki muhimu.
Kwa
mfano, wakati ambapo huko Norway kuna madaktari, manesi na wakunga 218
wa kuwahudumia watu 10,000 uwiano ni 1 kwa kila wahitaji huduma 10,000
kule Somalia. Mwezi huu, UNICEF inazindua kampeni kote duniani ya Every
Child ALIVE (Kila Mtoto Abaki HAI), ambayo inataka na kutoa suluhisho
kwa ajili ya watoto wachanga wa ulimwengu. Kupitia kampeni hiyo, UNICEF
inatoa wito wa haraka kwa serikali, watoa huduma za afya, wafadhili,
sekta binafsi, familia na biashara kuhakikisha kila mtoto anabaki hai.
“Kila mwaka, watoto wachanga milioni 2.6 kote duniani huwa hawaishi
zaidi ya mwezi wao wa kwanza. Watoto milioni moja hufa siku ileile
wanapozaliwa,” alisema Fore.
"Tunajua
kwamba tunaweza kuokoa uhai wa watoto walio wengi miongoni mwa hawa kwa
suluhu rahisi na matunzo bora ya afya kwa ajili ya kila mama na kila
mtoto mchanga. Hatua chache ndogondogo kutoka kwa kila mmoja wetu
zinaweza kusaidia kuhakikisha kunakuwa na upigaji hatua kwa kila uhai
mpya wa watoto hawa wachanga.” Nchini Tanzania, kampeni ya mwaka mzima
imepangwa ili kusaidia upazaji sauti kuhusu masuala yanayohusua akina
mama na watoto wachanga nchini. Lengo litakuwa ni kuunda vuguvugu la
kitaifa kuhusiana na suala hili, kwa kulenga vijana walio kwenye balehe
na walio hatarini zaidi, wanawake wajawazito na wanawake wanaonyonyesha.
No comments:
Post a Comment