SERIKALI
ya Awamu ya Tano inaingia katika mwaka wa pili wa utekelezaji wa Mpango
wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano wa mwaka 2016/17-2020/21
unaojikita katika ujenzi wa uchumi wa Viwanda na hivyo kufikia nchi ya
kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Uamuzi
wa Serikali wa kujenga uchumi wa viwanda umelenga katika kuleta
maendeleo jumuishi na endelevu kwa kutumia rasilimali zilizopo na hivyo
kuchangia katika pato la taifa pamoja na kutoa nafasi nyingi na endelevu
za ajira.
Ili
kufikia malengo hayo juhudi mbalimbali zimefanywa na Serikali na
mojawapo ya juhudi hizo ni kuandaa Mkakati wa Taifa wa Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi (NMSFEE) unaotekelezwa na Wizara na Taasisi zake;
Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Sekta
Binafsi pamoja na Wadau wa Maendeleo.
Utekelezaji
wa Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi unasimamiwa na Baraza la Taifa
la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) ambalo ni chombo cha juu kitaifa
cha kusimamia, kufuatilia na kuratibu utekelezaji wa shughuli
zilizoainishwa katika ya Sera ya Taifa ya Uwezeshaji wa Wananchi
Kiuchumi ya mwaka 2004.
NMSFEE
unatekelezwa kupitia Mwongozo ulioandaliwa ili kutoa maelekezo ya namna
ya kutekeleza ikiwemo uratibu, usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya
utekelezaji wa sera katika ngazi na sekta zote za kiuchumi.
Kupitia
NMSFEE mfumo wa uratibu wa uwezeshaji umepangwa kwa kuwa na kamati
kuanzia ngazi ya Taifa hadi kijiji/mtaa na kila kamati ikiwa na majukumu
yake kwa mtiririko endelevu.
Mkakati
wa NMSFEE imeanisha sekta mbalimbali ikiwemo mifuko ya uwezeshaji,
skimu za umwagiliaji, miundombinu ya barabara, miundombinu ya masoko,
huduma ya nishati vijijini, huduma za maendeleo ya biashara, hali ya
biashara, urasimishaji wa ardhi, mafunzo ya ujasiriamali, na maendeleo
ya vikundi vya kifedha vya kijamii.
Katika
kusimamia utekelezaji wa Mkakati huo, mwezi Julai mwaka huu Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa alizindua Mwongozo wa utekelezaji wa NMSFEE katika
kupanga, kutekeleza na kutathmini mipango na miradi mbalimbali ya
uwezeshaji wananchi kiuchumi hapa nchini
Taarifa
ya Serikali kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
(NEEC) inasema kuwa hadi kufikia Aprili 2017, Baraza limeweza kuendesha
mafunzo kwa waratibu wa dawati la uwezeshaji wananchi kiuchumi katika
halmashauri na mikoa, maafisa mipango na Wakurugenzi wa Halmashauri.
Mafunzo
hayo yalilenga kuwajengea uwezo watendaji hao kufahamu wajibu na
majukumu yao katika kusimamia na kuratibu utekelezaji wa mipango ya
uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Aidha
mafunzo hayo yaliyowahusisha Wakuu wa Mikoa na Wilaya yaliweza pia
yalitoa elimu kukuhusu miongozo ya kuanzisha, kuandikisha na kuendesha
vikundi vya kifedha vya kijamii pamoja na Mwongozo wa ukusanyaji na
utoaji wa taarifa za uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Pia,
waratibu wa uwezeshaji katika wizara na taasisi za Serikali wamepatiwa
mafunzo hayo ili kusimamia kwa karibu utekelezaji, kuratibu, kukusanya
na kutoa taarifa za utekelezaji wa mipango na miradi ya uwezeshaji
wananchi kiuchumi katika maeneo yao.
Ushiriki
wa wananchi katika shughuli za uchumi wa kisasa ni duni, hivyo kupitia
Mkakati wa NMSFEE ni wajibu wa sekta binafsi, Serikali na wadau wa
maendeleo kutoa nafasi kwa makundi yote kujiendeleza kikamilifu ili
kuwajengea mazingira mazuri ya ujenzi wa uchumi imara unaoweza kuhimili
ushindani katika soko la dunia.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, (NEEC), Beng’ Issa.
No comments:
Post a Comment