Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akisisitiza
jambo mbele ya wajumbe wa Bodi ya Kampuni ya Simu ya TTCL katika hafla
ya uzinduzi rasmi wa Bodi hiyo leo Jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto
ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya
Mawasiliano) Dkt. Maria Sasabo na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Omary
Nundu.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Kampuni ya Simu za Mkononi ya TTCL Mhandisi, Omary Nundu
akielezea jambo wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa Bodi hiyo leo
Jijini Dar es Salaam. Katikati ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Sekta
ya Mawasiliano) Dkt. Maria Sasabo.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya
mawasiliano) Dkt. Maria Sasabo akizungumza katika hafla ya uzinduzi
rasmi wa Bodi ya Kampuni ya Simu ya Mkononi ya TTCL leo Jijini Dar es
Salaam. Kutoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TTCL, Bw. Waziri
Kindamba, Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Mhandisi Omary Nundu na Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa.
Baadhi
ya wajumbe wa Bodi ya TTCL wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (hayupo pichani) wakati
wa hafla ya uzinduzi rasmi wa Bodi hiyo leo Jijini Dar es Salaam.Picha na Frank Shija – MAELEZO
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Mkame Mbarawa ameitaka Bodi
Mpya ya Wakurugenzi ya kampuni ya mawasiliano nchini (TTCL) kuhakikisha
kuwa inasimamia vyema kazi na majukumu yake ili kuiwezesha kampuni hiyo
kujiendesha kibiashara na kuimarisha huduma za mawasiliano hapa nchini.
Wito
huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo
ambapo aliwasisistiza kuwa wachape kazi ili kurahisisha huduma
mbalimbali za kimawasiliano hapa nchini na kuhakikisha kuwa wanaendana
na kasi ya serikali ya awamu ya tano yenye sera ya hapa kazi tu.
“Nataka
bodi mjue tunakwenda wapi katika kampuni hii lakini pia tunahitaji
kufanya kazi kwa juhudi, kushindana na makampuni mengine ya simu,
mhakikishe mapato makubwa yanatoka kwenye data halikadhalika tujue
mnapaswa mjue strenght (nguvu) yenu iko wapi maana tusipojibu maswali
haya hatuwezi kufanya ushindani na makampuni mengine,” alifafanua Prof.
Mbarawa.
Aidha
Prof. Mbarawa alisema kuwa, Serikali imeweka sera nzuri za uwekezaji
katika sekta ya mawasiliano kiasi ambacho kimeongeza mapato pamoja na
ushindani wa huduma ya mawasiliano na kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi
na maendeleo hapa nchini.
Prof.
Mbarawa aliongeza kuwa serikali imefanya mabadiliko yaliyofanywa na
serikali ili kuipa nguvu Kampuni ya TTCL ikiwa ni pamoja na kuondoa ubia
wa umiliki wa TTCL na wawekezaji asilimia 35 na kuzirejesha serikalini,
kujenga mkongo wa taifa wa mawasilino, kujenga kituo cha taifa cha
kuhifadhi kumbukumbu (Data center) pamoja na kulipa madeni ya kampuni
hiyo.
Aidha
Prof. Mbarawa ameitaka Bodi ya Wakurugenzi kuhakiksha kuwa TTCL inaleta
mabadliko na maendeleo katika kufikia sera ya serikali ya awamu ya tano
ya Tanzania ya viwanda, kuongeza wateja na watumiaji wa huduma
zitokanazo na TTCL, kuwafikia watumiaji wengi zaidi nchini kote na
kuendelea kuwa kampuni bora ya mawasiliano.
Prof.
Mbarawa aliongeza kuwa, TTCL ni lazima wabadilike katika utoaji wa
huduma zake, ili kuendana na manadiliko ya teknolojia ambapo amewaeleza
kuwa kwenye sekta ya mawasiliano mambo yanabadilika kila siku, sekta
inakua haraka na hata uendeshaji wake unabadilika.
“Mathalani
ukiangalia makampuni makubwa kwa sasa, mapato yao yamebadilika kutoka
kwenye sauti hadi data pamoja na miamala ya pesa hivyo TTCL wanapaswa
wajipime waangalie uwezo wao uko wapi na nguvu zao ziko wapi ili waweze
kujipanga vizuri kuhakikisha wanashindana na makampuni mengine ya
mawasiliano hapa nchini,” alifafanua Prof. Mbarawa.
Awali
akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi
Mhandisi Omary Nundu, alisema kuwa tangu ateuliwe katika bodi hiyo mambo
mengi wameyafanya hadi sasa ikiwemo kuifufua kampuni hiyo,
kushirikiana na wadau wengine wa mawasiliano pamoja na kuanzisha TTCL
Pesa.
“Kwa
sasa tunahudumia watu laki tatu hapa nchini, lakini tumenuia mwisho wa
mwaka huu wa fedha 2017/2018 tufikie wateja milioni moja na baada ya
miaka mitano yaani ifikapo 2021/2022 tuwe na wateja milioni tano ambapo
tutakuwa tumefikia asilimia 10 ya wateja wa soko la mawasiliano hapa
nchini,” alifafanua Mhandisi Nundu.
Aidha,
Mhandisi Nundu aliendelea kusema kuwa mwaka 2016, TTCL ilipata bilioni
0.21 katika soko lake na zaidi mwaka huu wanatarajia kupata bilioni 0.3
na kwamba wanatarajia kupata faida ya zaidi ya bilioni 40 ifikapo 2022
baada ya makato ya kodi.
“Katika
kuyafanikisha matarajio yote haya, tunapaswa kupata jumla ya dola za
kimarekani milioni 673, ambapo dola milioni 300 tunatarajia kuzipata
kama mtaji wa uwekezaji kutoka serikalini, huku kampuni ikitafuta njia
nyingine za kuapata fedha zilizobaki katika mpango na matarajio yetu,”
alifafanua Mhandisi Nundu.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa Mawasiliano Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na
Mawasiliano Dkt. Maria Sasabo alisema sekta ya mawasiliano ni kiungo
muhimu katika kukuza uchumi kwa kurahisisha mawasiliano ya kati ya mtu
na mtu na taifa kwa ujumla kwa kurahisisha usambazaji na upatikanaji wa
huduma na bidhaa kutoka sehemu moja na nyingine.
“Sera
ya serikali ya kuelekea uchumi wa viwanda inatoa fursa kubwa kwa sekta
ya mawasiliano kukua, pia ukuaji wa shughuli za uchumi unachochea
mahitaji ya mawasiliano kuongezeka ikiwemo serikali mtandao, tiba
mtandao, elimu mtandao, biashara mtandao, utangazaji mtandao kwa njia ya
runinga na radi,” alifafanua Dkt.Sasabo.
Bodi
ya Wakurugenzi ya TTCL iliteuliwa rasmi mwezi Februari 2017,na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ikiwa ni
jitihada za kufufua na kurejesha kampuni hiyo katika ushindani,
kusimamia mawasiliano yote ya serikali na kujiendesha kwa faida. Kwa
sasa serikali inajiandaa kupeleka muswada bungeni ili kuirasimisha TCCL
iwe na bajeti ya kujitegemea.
No comments:
Post a Comment