Mashindano
ya mpira wa Miguu maarufu kama URIO CUP 2017 yamezinduliwa rasmi Jijini
Dar es Salaam. Mashindano hayo, yanayoratibiwa na Msonge Africa Kwa
kushirikiana na Jomo International na kudhaminiwa na Times FM, yana
lengo la kuzikutanisha timu 32 zinazotokea katika sehemu mbalimbali za
Mkoa wa Dar es Salaam ili kuleta hamasa katika kata ya Kunduchi na pia
kuzipa timu za kata hiyo uzoefu.
Akizindua
mashindano hayo, Diwani wa Kata ya Kunduchi, Michael Urio ambaye ndio
mdhamini na mwanzilishi wa kombe hilo la Urio Cup alisema hii ni mara ya
pili kwa mashindano hayo kufanyika kwani mara ya kwanza yalifanyika
mwaka 2015 na kuhusisha timu 16 na kuongeza kuwa Urio Cup mwaka huu
inaenda sambamba na Kampeni maalumu ya ‘Wezesha Mama na mtoto Mpya wa
Kuncuchi’ ambayo ilizinduliwa hivi karibuni na yenye lengo la kuboresha
zahanati ya Ununio na Mtongani. Diwani
wa Kata ya Kunduchi, Michael Urio akipiga danadana ikiwa ni ishara ya
uzinduzi wa Urio Cup mashindano ambayo yanatarajiwa kufanyika katika
kata yake kuanzia mwezi ujao. Wengine kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa
Radio Times FM, Rehure Nyaulawa, Mratibu wa Urio Cup, Deus Buhilo na
Katibu wa Ligi na Mashindano wa Chama Cha Mpira Wilaya ya Kinondoni,
Khalid Shehani.
“Moja
ya ahadi nilizotoa kwa wananchi wangu ni kuimarisha sanaa na michezo
kwani michezo sasa hivi ni chanzo kikubwa cha ajira hasa kwa vijana.
Urio Cup iliyopita ilitoa baadhi ya wachezaji waliojiunga na timu za
daraja la kwanza na nimefahamishwa kuwa kuna wengine pia wanacheza ligi
kuu,” alisema Mh. Urio.
Alitoa
wito kwa wadau mbalimbali wapenda michezo wamuunge mkono katika hili
ili kombe hili liweze kukua mwaka hadi mwaka na kuwafadisha vijana wengi
zaidi. “Nimearifiwa kuwa tutawaalika wawakilishi kutoka timu za ligi
kuu ili waweze kutafuta vipaji kutoka kwa timu zitakazoshiriki Urio
Cup.
Hili
litasaidia sana katika kuamsha ari ya vijana huku wote wakiwa na
matumaini ya kusajiliwa na timu kubwa siku moja,” alisema diwani huyo.
Naye mratibu wa Urio Cup, Bw. Deus Buhilo alisema maandalizi yote
yamekamilika na wanatarajia kushindanisha timu 32 ambazo zinatakiwa
kujisajili na kulipia ada ya Tsh 70,000 na timu zinazotakiwa kujisajili
zinatakiwa kutuma maombi na kupata maelekezo kupitia namba 0652559122 na
malipo kupitia namba 0628555333.
Diwani
wa Kata ya Kunduchi, Michael Urio akizungumza wakati wa uzinduzi wa
Urio Cup mashindano ambayo yanatarajiwa kufanyika katika kata yake
kuanzia mwezi ujao. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Radio Times FM,
Rehure Nyaulawa na Katibu wa Ligi na Mashindano wa Chama Cha Mpira
Wilaya ya Kinondoni, Khalid Shehani.
“Urio
Cup ni mashindano makubwa na tumeweka vigezo ili kuhakikisha tunakuwa na
mashindano bora yanayofuata kanuni zote za FIFA na TFF. Tunataka
kuwajengea vijana wetu uzoefu ili waweze kufika katika ngazi za juu
zaidi,” alisema mratibu huyo na kumshukuru Diwani Urio kwa kuanzisha
mashindano hayo.
Alisema
mechi zitachezwa katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Tegeta na zitaanza
katika hatua ya mtoano nyumbani na ugenini na mshindi ndiye ataendelea
katika hatua inayofuata huku fainali za mashindano hayo yakifanyika
Katika Uwanja wa Machava uliopo Kunduchi Beach ambao kwa sasa umeanza
kufanyiwa matengenezo.
Alisema
mshindi wa kwanza atajinyakulia Tsh 3,000,000 na kombe, wa pili
1,500,000, timu yenye nidhamu Tsh 100,000, mfungaji bora Tsh 100,000,
Kikundi bora cha ushangiliaji Tsh 100,000, kipa bora Tsh 100,000 na
mchezaji bora (man of the match) Tsh 10,000 na kuongeza kuwa timu
zitakazotinga katika hatua ya 16 bora zitapata jezi.
“Mashindano
haya yatafanyika kwa miezi mitatu kuanzia Agosti 7 na tunatoa wito kwa
timu mbalimbali zijitokeze kujisajili na wakazi wa Dar es Salaam
wajitokeze kwa wingi pia kufuatilia,” alisema huku akiongeza kuwa
kiingilio katika kila mechi ni Tsh 500 ili kuhamasisha watu wengi zaidi
kupata nafasi ya kutazama mashindano hayo. Naye
Katibu wa Kamati ya Ligi na Mashindano wa Chama Cha Mpira Wilaya ya
Kinondoni (KIFA), Khalid Shehani alitoa pongezi kwa Diwani Urio kwa
juhudi zake za kukuza mpira katika kata yake na kumhakikishia
ushirikiano mkubwa. “Hii ni hatua kubwa mno na TFF inaunga mkono hatua
hizi asilimia 100 na tutatoa ushirikiano mkubwa ili kwa pamoja
tuendeleze mpira wetu.
Timu
zitakazoshiriki zijiandae vizuri na kuyapa mashindano haya umuhimu
mkubwa kwani ni ngazi ya kufika katika hatua nyingine za juu zaidi,”
alisema na kuomba timu zitakazoshiriki kuzingatia kanuni na taratibu
zote za mpira ili kuepukana na matatizo.
No comments:
Post a Comment