* DC Gondwe aeleza azma ya kuipeleka kasi miradi inayoiingizia Manispaa mapato
MKUU
wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe amesema katika kipindi hiki cha
mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan miradi yote inayoiingizia fedha
Manispaa hiyo itapelekwa kasi ili wananchi waweze kunufaika na juhudi za
Serikali na viongozi katika kuleta maendeleo.
Akizungumza
wakati wa kukabidhi mradi wa ujenzi wa uwanja wa mpira maalum kwa
Manispaa hiyo unaojengwa Mwenge jijini Dar es Salaam kwa mkandarasi
ambaye ni Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Gondwe amesema, mradi huo
utawanufaisha wakazi wa maeneo jirani kupitia vitega uchumi vilivyo
ndani ya uwanja huo.
Gondwe
amesema maeneo ya kimkakati ya kupaisha Manispaa hiyo ni pamoja na
mradi wa kituo cha mabasi Mwenge na uwanja wa mpira ambao Manispaa hiyo
ina timu ya mpira ya KMC ambayo inafanya vizuri katika Ligi kuu ya NBC
na kupitia uwanja huo wa nyumbani wakazi wa jirani watanufaika kupitia
maduka na vitega uchumi vilivyopo katika uwanja huo.
Kuhusiana
na ujenzi wa kituo cha mabasi Mwenge mradi wenye thamani ya shilingi
Bilioni 7 Gondwe ameeleza, kuna mpango kabambe wa kuwapanga wamachinga
katika eneo hilo lenye maduka yapatayo 146 ili waweze kufanya shughuli
zao za kiuchumi na kijiingizia kipato.
''Niwaombe
majirani zetu wa hapa panapojengwa kiwanja cha mpira waendelee kumpa
mkandarasi ushirikiano ili kazi ikamilike kwa wakati na tuanze kuingiza
mapato katika Manispaa yetu.'' Amesema.
Amesema
JWTZ watafanya kazi hiyo usiku na mchana katika kuhakikisha mradi huo
unakamilika ndani ya muda uliopangwa na hiyo ni pamoja na kuhakikisha
miradi yote inayoiingizia fedha Manispaa hiyo inakamilika kwa wakati.
Awali
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Songoro Mnyonge amesema ujenzi
wa uwanja wa mpira maalum kwa Manispaa hiyo uliopo Mwenge utakamilika
ndani ya miezi sita ijayo na tayari kampuni ya Azam Media imeahidi
kufunga taa zitakazowezesha mechi za usiku bure ikiwa watamaliza ujenzi
huo ndani ya muda wa miezi sita.
Songoro
amesema, kituo cha mabasi Mwenge kitakabidhiwa kwa mkandarasi mwingine
kwa hatua za umaliziaji na kinategemewa kukamilika ndani ya siku kumi.
''Miradi
ya maendeleo kinondoni ni mingi na tunaenda na kasi ya Mh. Rais katika
kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma zote muhimu, tutaendelea
kushirikiana na jeshi katika miradi mingine itakayopatikana hivi
karibuni ili iweze kutekelezwa kwa kasi.'' Amesema.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Bi. Khanifa Suleiman
amesema kuwa miradi hiyo miwili inatekelezwa kwa fedha zitokanazo na
mapato ya ndani na imelenga kuinua kipato cha wananchi kupitia maduka 70
yaliyopo katika uwanja huo pamoja na maduka 146 yaliyopo katika kituo
cha mabasi Mwenge ambapo wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga
watapangwa kwa utaratibu maalumu na kufanya shughuli zao za kujiongezea
kipato.
Bi.
Khanifa amesema Manispaa ina fedha za kutosha za kukamilisha miradi
hiyo ambayo imelenga kuwanufaisha watanzania na tayari JWTZ wapo kazini
katika kukamilisha miradi hiyo.
Akieleza
kuhusu utekelezaji wa mradi huo mkandarasi anayesimamia mradi huo Mkuu
wa Kikosi 361 Kanali David Luoga amesema mradi huo una thamani ya
shilingi bilioni 1 na milioni 200 na utakamilika kwa wakati ikiwa pande
mbili zitashirikiana katika kuleta maendeleo hayo.
Mkuu
wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe akizungumza na wanahabari
kuhusiana na miradi miwili ya kimkakati inayotekelezwa Mwenge jijini Dar
es Salaam na kueleza kuwa wataenda na kasi ya Serikali ya awamu ya sita
katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Msimamizi
wa mradi wa uwanja wa mpira wa Mwenge Kanali David Luoga akizungumza na
wanahabari kuhusiana na mradi huo na kueleza kuwa watashirikiana na
Manispaa hiyo katika kuhakikisha unakamilika kwa muda uliopangwa.
Mstahiki
Meya wa Manispaa ya Kinondoni Songoro Myonge (katikati,) akizungumza na
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe (kulia,) na Mkurugenzi wa
Manispaa ya Kinondoni Bi. Khanifa Suleiman (Kushoto.)
Mkuu
wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe (Kushoto) akiteta jambo na
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Songoro Mnyonge na mkandarasi wa
mradi huo Kanali David Luoga (katikati) Mkuu wa Kikosi 361.
Muonekano wa uwanja.
No comments:
Post a Comment