Serikali imesema ujenzi wa Daraja
jipya la Wami lenye urefu wa mita 513.5 na barabara za maingilio (km
3.8), unatarajiwa kuandika historia mpya kwa sekta ya Ujenzi mradi
kukamilika kabla ya muda uliopangwa kwenye mkataba.
Ujenzi huu
ulioanza mwezi Oktoba, 2018 unatarajiwa kukamilika mapema ifikapo mwezi
Julai, 2022 badala ya mwezi Novemba kama ilivyo kwa mujibu wa mkataba
wake.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof.
Makame Mbarawa, wakati akishuhudia ukamilikaji wa sehemu ya kupita
magari (deck) kwenye daraja hilo jipya ambalo ujenzi wake umefikia
asilimia 77.
"Hii
ni hatua kubwa sana kwa Daraja la aina hii, nimejionea linaendelea
vizuri na naamini kutokana na kasi aliyonayo mkandarasi kwa hakika
daraja hili litakamilika kabla ya muda", amesema Prof. Mbarawa.
Prof.
Mbarawa amefafanua ongezeko la magari katika Daraja la Wami la zamani
na wembamba wa daraja hilo umesababisha Serikali kujenga daraja kubwa
litakaloruhusu magari mawili kupita kwa wakati mmoja na hivyo kupunguza
Ajali zilizokuwa zikitokea Darajani hapo.
Aidha, Prof. Mbarawa
amemtaka mkandarasi kuongeza kasi na kuhakikisha anakamilisha kazi
zilizobakia ndani ya muda uliopangwa kwa kufanya kazi usiku na mchana
pia kuongeza rasilimali watu na mitambo.
Waziri Prof. Mbarawa
ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutoa fedha kwa
miradi mikubwa inayoendelea ili iweze kukamilika kwa wakati.
"Serikali
itaendelea kuwalipa Mkandarasi na Mhandisi Mshauri kulingana na madai
yanayowasilishwa na kuthibitishwa", amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Kwa
upande wake Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania,
Mheshimiwa Balozi Mingjian Chen, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa
kuendelea kuziamini kampuni za kichina katika utekelezaji wa miradi
mikubwa inayoendelea na amefurahishwa kuona kuwa miradi hiyo imekuwa
ikitoa fursa kwa wazawa kupata mafunzo wakati wa utekelezaji wa miradi
hiyo.
"Mradi huu umeajiri zaidi ya Watanzania 400 ambao bila
shaka wamepata ujuzi mkubwa na itasaidia kukuza uchumi wa ndani",
amesisitiza Balozi Chen.
Awali akitoa taarifa ya mradi Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Rogatius Mativila,
ameeleza kuwa ujenzi wa Daraja Jipya la Wami unagharamiwa na Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100 kwa jumla ya Shilingi
Bilioni 75.13.
Amebainisha gharama hizo ambazo zinahusisha
gharama za ujenzi ni Shilingi Bilioni 67.779, gharama za usimamizi wa
Ujenzi ni Shilingi Bilioni 6.307, Gharama za kazi ya Usanifu ni Shilingi
Milioni 852.991 na fidia kwa wananchi ni Shilingi Milioni 194.718
Eng.
Mativila ameongeza kuwa mradi huo umetoa jumla ya ajira 420, kati ya
hizo ajira 395 zimetolewa kwa watanzania na ajira 25 ni za wageni.
"Ni
matarajio yangu kuwa Watanzania wataalamu waliopata ajira na mafunzo
kwenye Mradi huu watasaidia kuongeza ujuzi kwa wajenzi na wasimamizi
wetu wa ndani ili hatimaye tuweze kutekeleza miradi kama huu kwa kutumia
Makandarasi wetu wa ndani", amesisitiza Mativila.
Ujenzi wa
Daraja Jipya la Wami una lengo la kutatua changamoto zilizokuwepo katika
Daraja la zamani kutokana na kutokidhi mahitaji ya watumiaji wa daraja
hilo tangu lilipojengwa Mwaka 1959.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
Muonekano wa hatua za ujenzi wa Daraja jipya la Wami lenye urefu wa mita 513.5 na barabara za maingilio zenye urefu wa kilometa 3.8 mkoani Pwani ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 77.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akiwa na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Balozi Mingjian Chen, wakiwasili mkoani Pwani kwa ajili ya kushuhudia utekelezaji wa ujenzi wa Daraja jipya la Wami (m 513.5), ambao umefikia asilimia 77.
Mwakilishi wa Msimamizi wa mradi wa Daraja jipya la Wami (m 513.5), Young Cheol Cheon, akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, wakati akikagua utekelezaji wake, mkoani Pwani.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akifafanua jambo kwa Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Balozi Mingjian Chen, kuhusu ujenzi wa Daraja jipya la Wami (m 513.5), ambapo sehemu ya kupita magari imemalizika kuunganishwa, mkoani Pwani.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, akiwa na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Balozi Mingjian Chen, wakikagua sehemu ya kupita magari (deck), iliyokamilika kuunganishwa katika Daraja jipya la Wami lenye urefu wa mita 513.5, mkoani Pwani.
Picha ya Pamoja ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Balozi Mingjian Chen, pamoja na viongozi wengine mara baada ya kukagua utekelezaji wa ujenzi wa Daraja jipya la Wami, mkoani Pwani.
No comments:
Post a Comment