Chama
cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania - Zanzibar (TAMWA, ZNZ),
kinashukuru kwa dhati maamuzi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi ya kuunda Wizara maalum
itakayoshughulikia pamoja na mambo mengine, masuala ya Wanawake na kwa
muktadha huo, kuwa ni Wizara inayojitegemea, nje ya Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii kama ilivyokuwa awali.
Hali
hiyo itapelekea masuala ya wanawake kuweza kushughulikiwa kwa makini
zaidi ikiwa ni pamoja na kutengewa raslimali inazostahiki ili
kuhakikisha mipango, utekelezaji na ufuatiliaji unafanyika kama
inavyostahiki.
Pendekezo
la kuwa na Wizara za wanawake pekee, lilikuja katika mikutano ya
kimataifa ya wanawake hasa uliofanyika Nairobi mwaka 1985 kufuatia
dhuluma ambazo wanawake wamekumbana nazo na zilivyowafanya kuwa nyuma
katika nyanja za kimaisha, hivyo Wizara ya wanawake pekee ilishauriwa
ili inyanyue hali hizo za wanawake duniani kwa ujumla na nchi
zinazoendelea kwa upekee hasa kama Zanzibar ambayo imezongwa zaidi na
mifumo kandamizi dhidi ya wanawake na watoto wa kike.
TAMWA
- ZNZ pia kinampongeza Waziri Riziki Pembe aliyeteuliwa kuiongoza
Wizara hiyo kutokana na uwezo wake na uzoefu, TAMWA tunaamini ataweza
kuleta mabadiliko yanayostahiki.
Hivyo,
TAMWA ZNZ inapenda kumshauri Mh. Waziri kuweka mifumo madhubuti ya
kurikodi maendeleo ya wanawake katika nyanja za kiuchumi na kiuongozi
kwa vile bado hazijaratibiwa vizuri.
Hivi
sasa kuna jitihada nyingi za kuinua kipato cha wanawake lakini bado
hakuna mifumo mizuri kuonesha hasa mabadiliko yanayotokea na mapungufu
yaliyopo ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa. Kukiwa na takwimu maalum za
wanawake hao itakuwa ni rahisi kuonesha maendeleo yaliyofikiwa katika
kundi hilo muhimu ambalo linafanya zaidi ya asilimia 50 ya wakaazi wote
wa Zanzibar.
Pia
katika uongozi, takwimu za wanawake katika nafasi mbali mbali za
kiutendaji katika ngazi za kitaifa na shina zikiwemo kwenye Wakurugenzi,
miundo ya bodi/kamati za kiutendaji bado ni changamoto kuzipata pamoja
na kuwa nchi inatekeleza itifaki na maazimio mbali mbali ya kuleta usawa
wa kijinsia hasa katika uongozi.
Itifaki
ya Umoja wa Afrika (AU) ya mwaka 2003 na Jumuiya ya Kusini mwa Afrika
(SADC) ya mwaka 2008 zote zinahimiza asilimia 50/50 katika vyombo vya
maamuzi katika Nyanja zote hizo bila ya takwimu na mikakati maalum
haitakuwa rahisi kupima muelekeo wa nchi katika hilo.
Mwisho
tunamtakia kila la kheir Waziri wa Wanawake katika kutekeleza majukumu
yake na kuwaomba wadau wa wanawake na jamii kwa ujumla kumpa
mashirikiano ili kufikia malengo yaliyowekwa.
No comments:
Post a Comment