SERIKALI ya Saudi Arabia, imetekeleza hukumu ya kuwanyonga watu 81 ndani
ya saa 24 wakiwemo raia 7 wa Yemen na mmoja kutoka Syria kwa kosa la
kukutwa na hatia ya kujihusisha na makosa ya ugaidi pamoja na kuwa na
imani potofu.
Utekelezaji wa hukumu hiyo umevunja rekodi kwa kuwa mauaji ya watu wengi zaidi kwa wakati mmoja katika historia ya nchi hiyo, taarifa ambazo zimethibitishwa na Shirika la Habari la Saudi Arabia (SPA).
Idadi kubwa ya mwisho ya utekelezwaji wa hukumu ya kifo nchini Saudi Arabia, ilikuwa ni Januari 2016 ambapo watu 47 walinyongwa hadharani huku wengine 27 wakinyongwa mwaka 2020.
Serikali ya Saudi Arabia imekuwa ikikosolewa kutokana na sheria zake kuwa kandamizi katika masuala ya siasa na dini na kuminya haki za binadamu japo serikali hiyo imekuwa ikikanusha tuhuma hizo kwa kudai kuwa inalinda usalama kupitia sheria za nchi yake.
Shirika hilo la habari linasema kuwa watuhumiwa wote walipewa haki ya kuwa na wanasheria na kwamba walihakikishiwa kutendewa haki katika mashtaka yao chini ya sheria za Saudi Arabia.
Mnamo mwaka 2019, serikali iliwanyonga jumla ya raia wake 37, wengi wao wakiwa ni kutoka madhehebu ya Shia kwa madai ya kujihusisha na vitendo vya ugaidi.
Taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo ilinukuliwa na Shirika la Habari la Taifa la SPA, inasema watu hao walihukumiwa kwa kosa la kutekeleza mauaji ya wanaume, wanawake na watoto wasiokuwa na hatia pamoja na kushirikiana na makundi ya kigaidi ikiwemo ISIS pamoja na Al-Qaeda.
No comments:
Post a Comment