Na Amiri Kilagalila, Njombe
Halmashauri
ya mji Njombe imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni
368,550,000/= kwa vikundi 34 vya wanawake vijana na walemavu katika
kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2021/2022 huku shughuli kubwa za
wanavikundi hao zikiwa ni kilimo,ufugaji,ufundi ushonaji,kuosha magari
na biashara za duka.
Akiwasilisha
taarifa fupi ya utoaji wa mikopo hiyo mkuu wa Idara ya maendeleo ya
jamii halmashauri ya Mji Njombe Bi. Enembora Lema amesema kuwa vikundi
34 viliweza kutembelewa na kukidhi vigezo, ambapo vikundi 10 vya
wanawake vimepatiwa mkopo wa shilingi milioni 136, vikundi 18 vijana
mkopo wa shilingi milioni 208 laki 7 na 6 watu wenye ulemavu kiasi cha
shilingi milioni 23 na laki 8.
“Niwapongeze
sana wanavikundi wa Njombe. Asilimia kubwa ni wakopaji na warejeshaji.
Kuna maeneo mengi watu wanahangaika kwenye urejeshaji wa mikopo hii ila
kwa Njombe mmekuwa warejeshaji wazuri. Niwaombe sasa mkasimamie miradi
ili iwe endelevu.”Alisema Afisa Maendeleo ya Jamii.
Akizungumza
katika hafla ya utoaji wa mikopo hiyo makamu Mwenyekiti wa Halmashauri
ya Mji Njombe Mhe. Erasto Mpete amesema kuwa hali ya utoaji mikopo
katika Halmashauri imeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka na hii
inatokana na namna Halmashauri ilivyojipanga katika zoezi zima la
uchangiaji wa mapato na namna elimu ya ulipaji kodi ilivyowafikia
Wananchi Mjini Njombe.
“Niwaombe
sana mikopo mliyopatiwa ikatumike kwa matumizi yaliyoombewa kwani
kukiuka vigezo hivyo mnakwenda kinyume na sheria na kanuni za utoaji
mikopo kwani kikundi kitakuwa kimepoteza sifa ya ukopaji. Mikopo hii
inatakiwa pia iwasaidie na wengine hivyo niwaombe Idara ya Maendeleo ya
Jamii kufuatilia mikopo hii ili mfuko uwe endelevu” Alisema Mpete.
Baadhi
ya Taasisi zilizoshiriki kutoa elimu mbalimbali kwa wanavikundi hao
zimefurahishwa na muitikio wa Wananchi kuchangamkia fursa hiyo na
kuwataka Wananchi wanaolalamika kuacha na badala yake kutumia fursa ya
mikopo ya Halmashauri kupata mitaji ya kuendeshea shughuli za
ujasiriamali na kiuchumi.
Mwakilishi
kutoka Taasisi ya Kupambana na rushwa TAKUKURU Daniel Mntambo amesema
kuwa lengo la wao kushiriki katika hafla hiyo ya utoaji mikopo ni
kuhakikisha kuwa hakuna viashiria vyovyote vya rushwa vinavyokuwepo
katika zoezi zima la utoaji mikopo.Aidha Taasisi nyingine zilizoweza
kushiriki na kutoa elimu kwa wanavikundi hao ni pamoja na jeshi la
polisi kitengo cha usalama barabarani, ofisi ya Hakimu Mkazi Wilaya ya
Njombe na Ofisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU.
Baadhi
ya wawakilishi kutoka katika makundi mbalimbali ambao ndio wanufaika wa
mikopo hiyo likiwemo kundi la Walemavu Angela Kilasi,Herman Sanga
mwakilishi wa Vijana na Grace Mbwilo kwa upande wa Wanawake amesema kuwa
anaipongeza Serikali kwa kuweza kufikia makundi mbalimbali ya wahitaji.
“Naipongeza
Serikali kwa kuweza kutoa mikopo mpaka kwa sisi Walemavu.Walemavu
wengi wapo ila wamejificha hawatoki kwa sababu hawana vitu vya kuwatoa
ndani. Ila kupitia sisi tunaopata mikopo naamini wengi watakwenda kutoka
na tutakwenda kuwa mabalozi kuwa mikopo kwa walemavu
inawezekana.”Alisema Angela Kilasi mwakilishi wa Walemavu
Halmashauri
ya Mji Njombe imeendelea kutekeleza maagizo ya Serikali na kutekelza
sheria ya fedha ya Serikali za Mitaa kifungu cha 37(A) ambayo inazitaka
Halmashauri kutenga asilimia kumi ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya
kusaidia vikundi vya Wanawake,Vijana na Walemavu kwa kutoa mikopo isiyo
na riba.
No comments:
Post a Comment