A great place to access the latest news and information.

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Sunday, March 13, 2022

DC Tabora aiagiza TARI kuandaa utaratibu wa kupata mrejesho wa teknolojia zilizosambazwa kwa wakulima

 

MKUU wa Wilaya ya Tabora, Mhe. Dkt. Yahya Ismail Nawanda ameuagiza Uongozi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kuweka utaratibu wa kufanya tathmini na ufuatiliaji wa mapokeo ya teknolojia zilizokwisha sambazwa na kupata mrejesho kutoka kwa wakulima na wadau mbalimbali unaohakisi malengo ya taasisi kuona tija iliyopo katika uhaulishaji teknolojia.
Dkt. Nawanda alitoa agizo hilo katika hotuba yake aliyoisoma kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Batilda Buriani katika Siku ya Mkulima iliyoandaliwa kwa pamoja na Vituo vya TARI Tumbi na Kihinga, na kufanyika katika Kituo Mahiri cha usambazaji teknolojia bora za kilimo cha Fatma Mwasa kilichopo Ipuli mkoani Tabora.

Akiwahutubia wakulima walioshiriki katika Siku ya Mkulima, Dkt. Nawanda alieleza kuwa TARI kupitia vituo vyake 17 vilivyopo nchini vimetafiti na kuzalisha teknolojia mbalimbali za kilimo zenye manufaa makubwa kwa wakulima na wadau, na siku hii, wakulima waitumie kupata elimu sahihi kuhusiana na kilimo cha mazao mbalimbali pamoja na kujionea kwa vitendo vipando vya mazao vilivyopo katika shamba kituoni hapo.
“Pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na TARI katika utafiti wa kilimo hapa nchini, TARI mna jukumu la kusambaza teknolojia bora za kilimo za kutosha zitakazojibu hoja na changamoto za wadau wetu hususan wakulima pamoja na kuweka vifaa vya kupimia udongo na afya ya mimea na kutoa majibu papo kwa papo ili kusaidia kilimo chetu kiwe na tija kubwa,”alisema Dkt. Nawanda.

Aidha, Dkt. Nawanda aliipongeza TARI kwa kuona hitaji la wakulima na kuamua kuanzisha Kituo hiki mahiri cha usambazaji teknolojia cha Fatma Mwasa mkoani Tabora, kituo ambacho kinasaidia wakulima kwa nyakati zote wanapohitaji kupata elimu na teknolojia bora za kilimo, badala ya kusubiri Maonesho ya Nane nane ambayo hufanyika mara moja kwa mwaka.
“Tukio hili lililofanywa na TARI hapa mkoani Tabora la kuwa na siku maalum ya mkulima “Farmers Field Day” ni la kupongezwa sana. Shughuli hii ni kubwa na inalenga kutoa mchango katika kuboresha na kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuongeza tija katika mazao yanayozalishwa, na hivyo kutimiza agizo la Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , la kuongeza tija na uwekezaji katika kilimo,”aliongeza Dkt. Nawanda.

Kwa upande wa Maafisa Ughani, Dkt. Nawanda alisema hao ni daraja kubwa kati ya Watafiti wa teknolojia bora za kilimo na wakulima, kwani wana jukumu kubwa la kutoa elimu sahihi na kwa wakati kwa wakulima pamoja na kutoa ushauri kuhusiana na changamoto zinazowakabili wakulima, hivyo ni budi kila Halmashauri kuhakikisha wana maafisa ughani wa kutosha kwa ajili ya kuwasaidia wakulima, ila nao maafisaa ughani wanapaswa kwenda na wakati kwa kupata elimu kutoka TARI kuhusiana teknolojia bora za kilimo zilizofanyiwa utafiti, na waitumie elimu hiyo kuwanufaisha wakulima katika maeneo yao.
“Leo nimejifunza kuhusiana na teknolojia bora pamoja na kushuhudia kwa vitendo katika vipando vya mazao mbalimbali hapa Fatma Mwasa. Wakulima waliohudhuria nao bila shaka wamefaidika na siku hii muhimu. Maafisa ughani nao nashauri waje kupata elimu hapa TARI Tumbi. 

"Miongoni mwa teknolojia nilizojifunza ni pamoja na matumizi sahihi ya mbegu bora, kupanda kwa nafasi, matumizi sahihi ya mbolea na viuatilifu na njia mbadala za kurutubisha ardhi kwa kutumia miti na mimea jamii ya mikunde. Teknolojia nyingine ni mbinu bora za kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno na uongezaji thamani katika mazao,” alisema Dkt. Nawanda.
Katika hatua nyingine Dkt. Nawanda aliwashauri Viongozi wa mikoa ya Tabora na Kigoma wakiwemo Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya kutumia vizuri fursa ya kuwepo kwa Kituo cha Fatma Mwasa na kuhakikisha wakulima na maafisa ugani na wadau waliopo kwenye maeneo yao wanafika katika kituo hicho kwa ajili ya kupata mafunzo kwa vitendo ili kuongeza tija katika kilimo chao.

Kwa upende wake, Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Tumbi,Dkt. Emmanuel Mrema alisema lengo kubwa la kuwa na kituo hicho mahiri ni kutoa mafunzo ya kilimo bora kwa wadau kama vile matumizi sahihi ya mbolea, viuatilifu na kilimo hifadhi kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Pamoja na kutoa ushauri unaozingatia utunzaji wa mazingira kwenye shughuli za kilimo ili kuokoa muda na nguvukazi kwa kuwa na namna bora ya kuandaa mashamba, upandaji, palizi, uvunaji na usindikaji ili kuongeza ubora na thamani wwa bidhaa za mazao.

Nao baadhi ya wakulima waliohudhuria Siku ya Mkulima wameshukuru na kuipongeza TARI kwa uamuzi wa kutoa mafunzo na teknolojia mbalimbali ambazo zimeonyesha tija kubwa baada ya kuzitumia kwa kupata mazao mengi tofauti na kabla ya kuanza kutumia teknolojia za TARI.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages