Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi mfano wa hundi ya Shilingi Milioni
104 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dkt.
Julius Mwaiselage ambazo zimekusanywa kupitia CRDB Bank Marathon kwa
ajili ya kusaidia ujenzi wa Kituo cha Mawasiliano. Katika mbio hizo za
hisani Benki ya CRDB mwaka huu imekusanya Shilingi Milioni 500, ambapo
fedha nyengine Shilingi Milioni 200 zimetolewa kwa Taasisi ya Moyo ya
Jakaya Kikwete kwa ajili ya kusaidia gharama za upasuaji kwa watoto
wenye magonjwa ya moyo na fedha zilizobaki zimepelekwa katika kusaidia
kampeni kabambe ya mazingira nchini. |
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi hundi ya Shilingi Milioni 5 mshindi
wa kwanza wa mbio za 42km kwa upande wa wanawake katika CRDB Bank
Marathon, Shelmith Nyawira raia wa Kenya. Katika mbio hizo Benki ya CRDB
imekusanya jumla ya Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya kusaidia watoto
wenye upasuaji wa moyo JKCI, kujenga Kituo cha Mawasiliano Taasisi ya
Saratani Ocean Road na kampeni kabambe ya mazingira nchini, Mbio hizi
zimefanyika Jumapili katika viwanja vya farasi, Oysterbay, Dar es
salaam.
Akizungumza na washiriki, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mbio hizo, aliipongeza Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Benki ya CRDB kwa kufanikisha mbio hizo zilizokuwa na lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya watoto wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo JKCI, kujenga kituo cha mawasiliano cha Taasisi ya Saratani, Ocean Road (ORCI) na kusaidia utunzaji mazingira kupitia kampeni ya Pendezesha Tanzania.
Waziri Majaliwa alisema kuwa Serikali inasikia fahari kuona taasisi za kizalendo kama Benki ya CRDB zikiwa mstari wa mbele katika kusaidia Serikali kuboresha sekta za kijamii kama vile; afya, elimu na mazingira na huku akikiri kwa dhati kuwa mbizo hizo zinazofanyika kila mwaka kuwa ni fursa adhimu ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwekeza katika ustawi wa jamii.
“Nimekuja hapa kwa lengo la kuonyesha kuwa Serikali inaunga mkono na kufurahishwa sana na ubunifu huu wa Benki ya CRDB. Kwa niaba ya Serikali niwashukuru kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) kwa kuboresha huduma za afya kwa umma,” anaeleza Waziri Mkuu.
Aliwapa kongole viongozi mbalimbali wa Serikali ikiwamo; Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, Naibu Waziri mwenye dhamana ya Michezo, Pauline Gekul, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel na washiriki wengine wote kwa kuunga mkono jitihada hizo ambazo zimejielekeza katika kuokoa maisha ya wale wenye uhitaji katika jamii na kuboresha mazingira.
Alipongeza uamuzi wa Benki ya CRDB kuendelea kusaidia upasuaji wa watoto wenye magonjwa ya moyo. Waziri Mkuu alisema uamuzi huo utaendelea kusaidia kupunguza makali ya gharama kwa ajili ya upasuaji wa moyo ambazo watu wengi hawawezi kuzimudu pamoja na Serikali kutoa ruzuku ya asilimia 80.
“Wazo hili la kuendelea kusaidia gharama za upasuaji kwa watoto ni uamuzi mzuri sana kwani hata asilimia 20 iliyobaki wazazi wengi hawana uwezo wa kuchangia. Hongereni kwa kurejesha tabasamu kwa watoto nakuwapatia tumaini la maisha,” Waziri Majaliwa alisisitiza.
“Kati ya fedha zote Shilingi Milioni 500 zilizopatikana katika mbio hizo, Shilingi Milioni 200 zimeelekezwa JKCI, Sh104 milioni zimeenda ORCI na kiasi kilichobaki kimeelekezwa katika kampeni za utunzaji wa mazingira,” alisema Nsekela.
Katika maelezo yake ya kumkaribisha Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Mkurugenzi wa Mawasiliano Benki ya CRDB, Tully Mwambapa alisema asilimia 85 ya washiriki wa mbio hizo ni Watanzania huku akibainisha kuwa wakimbiaji wa kimataifa waliojisali kutoka nje ya Tanzania ni zaidi ya 700.
Akiongezea, Tully alisema mbio hizo za CRDB Bank International Marathon ambazo zimeendelea kutambulika kimataifa baada ya kupatiwa ithibati na World Athletics na AMIS, kwa sasa zina hadhi sawa na zile mbio za Sanlam Cape Town Marathon za Afrika Kusini na Boston Marathon za nchini Marekani.
Mbio hizo zimeendelea kupata mwamko mkubwa kutoka kwa wakimbiaji kutokana na lengo lake la kusaidia kusaidia jamii. Hii ni mara ya pili Benki ya CRDB inaandaa mbio hizi kwa mafanikio makubwa, baada ya zile zilizofanyika mwaka na kukusanya Shilingi Milioni 200 kwa ajili ya upasuaji wa watoto katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete. Mbio za mwaka jana zilizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye kwa wakati huo alikuwa akihudumu kama Makamu wa Rais.
Katika 10km, mshindi kwa upande wa wanaume alikuwa Joseph Tiophil raia wa Tanzania alitumia muda wa 00:28:51, kwa wanawake Transfora Musa raia wa Tanzania ameshika nafasi ya kwanza baada ya kutumia muda wa 00:33:52.
Katika mashindano ya mbio za baiskeli 65km, Masunga Duba raia wa Tanzania aliibuka mshindi kwa upande wa wanaume baada ya kutumia muda wa 01:49:07, upande wa wanawake Swabra Abdallah raia wa Tanzania ameibuka mshindi baada ya kutumia muda wa 02:06:39. Washindi 32 katika mbio hizo wamejizolea jumla ya Shilingi Milioni 50.
No comments:
Post a Comment