RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kupata chanjo ya afua ya maambukizi ya virusi vya UVIKO-19 (COVID-19) ni hiari ya mtu na imani yake katika kupata chanjo husika ili kujikinga na janga hilo.
Rais Samia ameyasema hayo alipozungumza katika uzinduzi wa chanjo hiyo nchini Tanzania, chanjo aina ya Johnson Johnson iliyofika nchini kwa zaidi ya dozi Milioni 1, iliyotolewa kwa ufadhili wa Watu wa Marekani.
Rais amesema chanjo hiyo haina madhara na hatari yoyote kutokana na kupata uthibitisho wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nchini chini ya Wataalamu wake wa masuala hayo ya Afya, amesema hadi sasa idadi ya wanaotaka kupata chanjo hiyo ni wengi na wasiotaka pia ni wengi.
“Miaka ya nyuma nilipokuwa Shule ya Msingi, nilipata chanjo nyingi sana kama Tano, na chanjo ya leo ni ya Sita”.
“Ndugu zangu Watanzania, mimi ni Mama wa Watoto Wanne na Wajukuu kadhaa, na ni Mke pia lakini kubwa zaidi ni Rais wa Tanzania, nisingekubali kuleta madhara kwa taifa langu ambalo naliongoza”, amesema Rais Samia.
Pia amesema chanjo hivyo imekuja kwa idadi ndogo lakini watajitahidi kuhakikisha inakuja kwa wingi ili kutoa fursa kwa wanaotaka kupata, ili ipatikane kwa urahisi, amesema amezungumza na Mkurugenzi wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Barani Afrika (Africa CDC), Dkt. John Nkengasong juu ya upatikanaji wa chanjo hiyo kwa idadi kubwa katika Jumuiya za Kimataifa.
Katika mazungumzo hayo, Rais amesema wamezungumzia suala la kuweka oda kwa Umoja wa Mataifa (UN) katika kupata idadi nyingine zaidi ya chanjo hiyo hapa nchini.
Rais Samia ametoa wito na kushauri kwa Wizara ya Afya na Mamlaka zinazoshirikiana kupambana na janga hilo, Vituo vya Runinga kutoa elimu ya kutosha kwa Jamii ya Watanzania katika kukabiliana na janga hilo tishio Ulimwenguni.
Pia, amewataka Wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya janga hilo la UVIKO-19. Amesema Mikoani wanataka kupata chanjo hiyo sambamba kuangalia uwezekano wa kupata zaidi kwa Jamii mbalimbali zinazoishi nchini wakiwemo Wafanyabiashara ili kupata urahisi wa kusafiri sehemu mbalimbali kufanya shughuli zao.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizindua Chanjo ya Uviko 19 katika Viwanja vya Ikulu Jijini Dar es salaam leo Julai 28,2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akionesha Cheti cha Uthibitisho wa Chanjo muda mfupi baada ya kuzindua Chanjo ya Uviko 19 katika Viwanja vya Ikulu Jijini Dar es salaam leo Julai 28,2021
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akipata Chanjo ya Uviko 19 katika Viwanja vya Ikulu Jijini Dar es salaam leo Julai 28,2021. Picha na Ikulu.
No comments:
Post a Comment