HERENI ni pambo linavoliwa masikioni na kwa kiasi kikubwa linachangia kuongeza mvuto na muonekano mzuri.
Kuna aina nyingi za hereni katika tamaduni mbalimbali. Zipo ambazo hutengenezwa kwa kutumia vito vya thamani kama vile Dhahabu, Almasi, Shaba au Kopa.
Vilevile zipo ambazo hutengenezwa kwa kutumia malighafi za asili kama vile ubao, vifuu vya nazi, mfupa kioo na shanga ambazo zimekuwa zikivaliwa sana na wanawake wa kimasai. Hereni zilizotengenezwa kwa shanga zimekuwa zikiwavutia watu wengi kuvaa kutokana na nakshi zake za asili.
Mara nyingi uvaaji wa hereni unatakiwa kuzingatia aina ya nguo uliyovaa, hapo unatakiwa kucheza na rangi. Mpangilio wako wa nguo na hereni hata na viatu utakufanya uonekane maridadi muda wote.
Unapotoka kwenda katika shughuli zako, au uwapo nyumbani basi zingatia uvaaji wa hereni na nguo. Uvaaji usiozingatia mpangilio wa rangi na hereni zako huondoa ladha ya urembo na si rahisi kwa mtu mwingine kugundua umependeza.
Licha ya kuwa hapo awali hareni zilikuwa zikivaliwa na wanawake pekee lakini miaka ya hivi karibuni tunaona urembo huu unaanza kuwavutia baadhi ya wanaume hususan vijana wa mjini.
Kutokana na hilo kuna hereni ambazo zimetengenezwa maalum kwa kuvaliwa na wanaume, hizi huwa za kubana na huwa na umbo dogo ukilinganisha zile zinazopendwa kuvaliwa na wanawake.
Angalizo: Epuka kuvaa hereni zaidi ya moja katika tundu la sikio kwani kufanya hivyo kunaweza kupelekea ukubwa wa tundu kuongezeka na hatimaye nyama ya sikio kuchanika. Hereni nzito sana nazo huchangia kutokea kwa tatizo hili.
No comments:
Post a Comment