A great place to access the latest news and information.

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Saturday, March 20, 2021

CCM KUKUTANA KWA DHARURA MACHI 20, 'TUMEMPOTEZA KIONGOZI MZALENDO ALIYEIPENDA NCHI YAKE'


Na Mwandishi Wetu, Dodoma | KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM Taifa itakutana kwa dharura siku ya Jumamosi Machi 20 mwaka huu katika Ofisi Ndogo za Chama hicho Lumumba mkoani Dar es Salaam kufuatia Kifo cha Rais Dk John Magufuli.

Akizungumza na wandishi wa habari Jijini Dodoma, Katibu wa Itifaki na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema baada ya Chama kupokea taarifa ya kifo cha Rais Dk Magufuli kilichotokea jana na kutangazwa na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan viongozi wakuu wa chama wameshauriana kukutana siku hiyo ya Jumamosi.

Polepole amesema Chama kimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Rais Dk John Magufuli ambaye pia alikua Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa huku akisema watanzania wana deni kubwa la kuyaenzi mambo makubwa na mazuri ya kihistoria yaliyofanywa na Rais Magufuli ndani ya kipindi kifupi cha takribani miaka mitano na miezi mitatu.

"Tumeshtushwa sana na taarifo za kifo cha Jemedari wetu, mzalendo halisi ambaye amelitumikia Taifa letu kwa moyo wa kipekee, tunaomba wanachama wetu na watanzania kwa ujumla kuungana na kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu kwetu sote. Tunawaomba watanzania kwa umoja wetu kutafakari mambo makubwa ya kihistoria yaliyofanywa na Rais wetu Dk John Magufuli ndani ya kipindi hiki kifupi, tuutafakari mchango wake wa kihistoria," Amesema Polepole.

Ameongeza kuwa shughuli zote za Chama hicho hasa zile za uchaguzi wa ndani zitasimama kwa muda huku pia kukiwa na maombolezo ya siku 21 Bendera za chama zikipepea nusu mlingoti lakini pia akitangaza kuwepo kwa kitabu cha Maombolezo kwenye Ofisi za CCM Makao Makuu Dodoma, Ofisi za CCM Kisiwa Ndui Zanzibar na Ofisi Ndogo za Lumumba Dar es Salaam.

Rais Dk John Magufuli amefariki jana Machi 17 majira ya saa 12 za jioni katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alipokua akipatiwa matibabu kufuatia kuwa na tatizo la mfumo wa umeme wa moyo.

Dk Magufuli amekua Rais wa Tanzania toka mwaka 2015 aliposhinda kwenye Uchaguzi mkuu na baadae kushinda tena katika kipindi chake cha pili mwaka jana (2020) huku pia akiwa Mwenyekiti wa CCM tangu mwaka 2016.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages