SIKU Moja baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutangaza wagombea wake wa Ubunge kwenye majimbo yote nchini, aliyekua Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof Kitila Mkumbo leo amechukua fomu ya kugombea Ubunge kwenye Ofisi ya Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo.
Prof Kitila amefika katika Ofisi za Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubunge kuchukua fomu hiyo akiambatana na Mgombea wa Jimbo la Kibamba (CCM), Issa Mtemvu ambapo wote wameahidi kufanya kampeni za kistaarabu.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu hiyo, Prof Kitila amekishukuru chama chake kwa kumteua kupeperusha bendera ya chama hicho Jimbo la Ubungo huku akiahidi kulirudisha CCM baada ya kushikiliwa na upinzani kwa muda mrefu.
Amesema anazifahamu changamoto zote zinazolikabili Jimbo hilo ikiwemo suala la maji, mama lishe na kuahidi kushirikiana na Serikali kuhakikisha kila mwananchi wa Ubunge anafaidika na Nchi yake.
" Niipongeze na kuishukuru Kamati Kuu ya Chama chetu na kipekee Mwenyekiti na Rais wetu, Dk John Magufuli kwa kuniamini na kuniteua, niwaahidi kwamba nimekuja Ubungo kufanya kazi na kuwatumikia wananchi wa hapa kwa uzalendo, uadilifu na uchapakazi.
Ninajua shida za hapa, ni jukumu langu kama Mbunge kushirikiana na serikali yetu ili kwa pamoja tulete maendeleo kwenye Jimbo letu, " Amesema Prof Kitila.
Pia amewaomba watanzania na wananchi wa Ubungo kumpigia kura nyingi za ndio, Rais Magufuli ili aweze kuendelea kuwaletea maendeleo kama alivyofanya kwenye miaka mitano ya mwanzo kwa kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa Nchi zenye uchumi wa kati.
Kwa upande wake Mgombea wa Ubunge Jimbo la Kibamba, Issa Mtemvu nae amemshukuru Rais Magufuli na Chama chake cha CCM kwa kumuamini na kumpa ridhaa ya kwenda kuwatumia wananchi wa Kibamba.
"Namshukuru Rais wangu Magufuli, Nakishukuru Chama na wajumbe wote kwa ujumla, Jimbo la Kibamba najua changamoto zao nyingi sana na haswa changamoto ya ukosefu wa maji, Mimi na viongozi wangu tutawatua ndoo akina mama wa Kibamba kwa sasa nisizungumze sana tukutane kwenye kampeni tukiwa na lengo la kurudisha Jimbo CCM na kuwatumikia wananchi," Amesema Mtemvu.
No comments:
Post a Comment