A great place to access the latest news and information.

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Tuesday, July 28, 2020

Diary ya Shigongo: Nenda Mkapa, Nenda Shujaa!

TAIFA linazizima! Mbuyu umeanguka katikati ya msitu mkubwa, miti mingine yote inatetemeka! Binafsi ninayo huzuni kubwa ndani ya moyo wangu kutokana na kifo cha Rais wa Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mzee wetu, Benjamin William Mkapa ambaye amefikwa na umauti usiku wa Alhamisi ya Julai 23, mwaka huu.

Rais Dk John Pombe Magufuli ndiye aliyetangaza habari za kifo hicho, majira ya saa sita za usiku na kulifanya taifa zima lizizime. Ama kwa hakika kifo ni fumbo kubwa sana ambalo binadamu tumeumbiwa!

Mzee Mkapa alikuwa mzima jioni ya siku hiyo, namnukuu Jakaya Mrisho Kikwete ambaye anasema; “Kifo ni siri ya Mwenyezi Mungu. Jana jioni nilipomuona hospitali tulizunguma sana. Alikuwa na maumivu, lakini si yale ambayo ukitoka kumuangalia mgonjwa unawaamia wenzako, eh, nimemuona mgonjwa lakini… Yalikuwa maumivu ya kawaida tu, tumezungumza zaidi ya saa nzima…”

Si hivyo tu, mbali na maelezo hayo ya Mzee Kikwete, sote tutakuwa mashahidi kwamba wiki moja iliyopita, Mzee Mkapa alishiriki kikamilifu katika mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), uliofanyika jijini Dodoma na alionekana kuwa na afya njema.

Kifo hakina huruma! Wengi tulitamani mzee wetu Mkapa aendelee kuwa nasi, lakini Mungu amempenda, hatuna cha kufanya zaidi ya kumuombea mwenyezi Mungu ampe pumziko la milele na kumsamehe dhambi zake!

Ukweli ambao watu wengi huwa hatupendi kuukubali ni kwamba kila binadamu aliyezaliwa, ipo siku atakufa na kuondoka hapa duniani. Mimi na wewe, sote njia yetu ni moja, hakika TUTAKUFA ingawa hakuna anayejua siku wala saa ya kuondoka kwake.

Jambo la msingi, ni kuacha alama katika maisha yako. Mzee Mkapa ameacha alama kwenye maisha yake ya hapa duniani na japokuwa leo hii hatunaye tena, bado mambo mengi makubwa aliyoyafanya yataendelea kuishi.

Ni ukweli usiopingika kwamba katika kipindi cha miaka kumi aliyokuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Mkapa alifanya mambo mengi sana mazuri ambayo yametufanya tufike hapa tulipofika leo kama Taifa.

Ni Mzee Mkapa huyu ndiye aliyeanzisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya rushwa hapa nchini na sote tutakuwa mashahidi wa jinsi taasisi hii inavyozidi kukabiliana na watu wote wenye tabia za kutoa au kupokea rushwa.

Katika uongozi wake, Mzee Mkapa alianzishwa mamlaka mbalimbali kama vile ya kukusanya mapato (TRA) ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato na hiyo ilikuwa ni Julai 1996. Miaka miwili baadaye, Julai 1998, akaanzisha mfumo wa VAT ambao unatumika mpaka leo.

Mamlaka zingine alizoanzisha ni Mamlaka ya Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Mamlaka ya Mafuta (EWURA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mamlaka ya Usafirishaji Nchi Kavu na Baharini (SUMATRA) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege.
Pia alianzisha Mamlaka za Maji Safi na Taka, Wakala wa Barabara (TANROADS) na kadhalika.

Nikukumbushe pia kwamba mzee Mkapa ndiye aliyeanzisha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, lakini pia ndiye aliyeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). Umuhimu wa vitu vyote hivi alivyovianzisha unajidhihirisha wazi na vimekuwa msaada mkubwa kwa marais waliofuatia baada yake.

Ni kama aliwachorea barabara ya kuelekea kwenye mafanikio na ndiyo maana kuanzia kipindi cha utawala wake, Tanzania inaendelea kupiga hatua kubwa za kimaendeleo, mpaka leo tunapojivunia kuingia kwenye uchumi wa kati chini ya Rais Magufuli.

Mambo mazuri aliyoyafanya mzee Mkapa ni mengi na hayahesabiki, itoshe tu kusema aliitumia vyema miaka yake kumi ikulu na hakika ameyabadilisha maisha ya watu wengi sana na kitu pekee tunachoweza kukifanya kwa sasa, ni kumpa heshima anayostahili kwa kumsindikiza vizuri kwenye safari yake ya mwisho lakini pia kuyaenzi yale yote mazuri aliyoyafanya.

Ndugu zangu, tumekua katika jamii ambayo mara zote tumekuwa tukiambiwa kwamba si jambo jema kumzungumzia vibaya marehemu hasa kutokana na ukweli kwamba anakuwa hana tena uwezo wa kujitetea.
Lakini maendeleo ya sayansi na teknolojia, huu utandawazi umewafanya baadhi ya watu kuwa kama ‘mafyatu’, wanasahau misingi na tamaduni zetu kama watoto wa mama mmoja, Tanzania.

Kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii, watakuwa wanaelewa kinachoendelea huko mitandaoni kwa baadhi ya watu wachache wasio na utu, ambao badala ya kumuombea pumziko la milele mzee wetu, wengine wapo ‘bize’ kushutumu mambo mbalimbali yaliyofanywa na mzee wetu Mkapa.

Yapo mambop mengi mazuri ambayo yalifanywa na mzee wetu huyu enzi za uhai wake, kabla hajawa rais, akiwa rais na baada ya urais lakini hilo lisifanye tusahau kwamba mzee wetu huyu naye alikuwa binadamu kama mimi na wewe!

Kuna mahali alifanya makosa kama binadamu na uzuri ni kwamba hata baada ya kuondoka madarakani, mara kadhaa aliendelea kukiri kwamba kuna mambo alikosea katika utawala wake na amekuwa akiijutia nafsi yake!
Ndiyo! Yeye ni binadamu na siyo malaika, alifanya mazuri mengi lakini kama binadamu wengine wote, alikuwa na mabaya yake ambayo mpaka anafikwa na mauti alikuwa akiyajutia.

Yapo mambo ambayo hayakuwafurahisha wengi, yapo mambo ambayo yaliwaumiza baadhi ya watu lakini kwa kuwa tumeumbiwa kukosea, ni matumaini yangu kwamba kila ambaye alikosewa, atamsamehe mzee wetu huyu ili akapate pumziko la milele badala ya kuendelea kuzungumza mambo ambayo ni kinyume na mila na desturi zetu na kinyume kabisa na ubinadamu.

Miongoni mwa mambo ambayo yaolikuwa yakimsikitisha kiasi cha kumfanya ayaandike kwenye kitabu chake cha My Life, My Purpose, ni pamoja na mauaji yaliyotokea Zanzibar Januari 26 na 27, 2001 ambapo wafuasi kadhaa wa Chama cha Wananchi (CUF) walipoteza maisha yao.

Mzee Mkapa ambaye hakuwepo nchini wakati mauaji hayo yanatokea, akiwa Davos, Uswisi wakati huo, anakiri katika kitabu chake kwamba yalimpa wakati mgumu sana na ni miongoni mwa mambo ambayo yamemfanya abaki na majuto makubwa katika maisha yake.

“Nilijutia mauaji haya. Najutia hadi leo,” ameandika katika kitabu chake. Hiyo pekee inatosha kuonesha ni kwa kiasi gani mzee wetu alikuwa muungwana! Alifanya makosa na akayatambua makosa yake, iweje leo hii itumike kama fimbo ya kuonesha kwamba hakuna lolote zuri alilolifanya kwenye maisha yake?

Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni! Alikosea na akakiri makosa yake, hakuna haja ya kuendelea mjadala huu. Makosa mengine ambayo mwenyewe anakiri kuyafanya ni pamoja na mchakato wa uuzaji wa mashirika ya umma na uuzwaji wa nyumba za serikali.

Haya yote ameyaeleza vyema kwenye kitabu chake! Huu ni uungwana wa hali ya juu, nawaomba wale ambao kwa namna moja au nyingine waliguswa na makosa haya, wamsamehe mzee wetu na kwa sasa sote tushikamane kumsindikiza katika safari yake ya milele.

Mzee Mkapa alikuwa shujaa wa taifa letu, akisimamia kauli mbiu yake ya ukweli na uwazi! Aliyoyafanya ni mengi sana ambayo nikisema nianze kuyataja moja baada ya jingine, ukurasa huu unaweza usitoshe. Somo kubwa ambalo anatuachia sote tuliobaki, ni kwamba tunapaswa kuacha alama kwenye maisha yetu.

Maisha ya Mkapa yalikuwa alama ya ushujaa na uthubutu mkubwa ambao leo ndiyo unaofanya tutembee vifua mbele kama Watanzania! Busara zake zilimfanya awe kimbilio la nchi nyingi zilizokuwa na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe, sote tunakumbuka jinsi mzee huyu alivyokuwa akitumika kusuluhisha migogoro kwenye nchi mbalimbali zinazotuzunguka.

Kifo chake siyo pigo kwa Tanzania pekee, bali Afrika nzima! Tumuombee mwenyezi Mungu ampe pumziko la milele.

Nenda Mkapa! Nenda mzee wetu! Kimwili haupo nasi lakini ndani ya mioyo yetu utaendelea kuishi. Natoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania kwa jumla kutokana na pigo hili, Mungu azidi kutupa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.
Mungu ailaze roho ya mzee wetu Mkapa mahali pema peponi. Amina!
Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages