Na Mwandishi wetu Tanga.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigela amepiga marufuku kitendo cha Madereva kupimwa kila mara katika Mpaka wa Tanzania na Kenya uliopo Holoholo Jijini Tanga.
Marufuku hiyo imetolewa leo Juni 17 na Mkuu huyo wa Mkoa wa Tanga kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri na kwamba ili kuwahepusha Madereva hao kupima mara kwa mara sasa watakuwa wakibadirishana Magari wafikapo Mpakani.
"Nitoe wito kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri kuweka Madereva katika nchi zote, kama una chombo cha usafiri uwe na Dereva Tanzania na Kenya wabadilishane Magari wafikapo hapa mpakani" alisema Shigela.
RC Shigela amechukua hatua hiyo ya kukataza Madereva wa Tanzania kupimwa mara kwa mara ili kuepuka taarifa za uongo kuhusu ugonjwa wa Corona nchini Tanzania hali inayoweza kuharibu ukuaji wa Uchumi wa Nchi.
"Tukiruhusu watu wetu waendelee kupimwa huenda kesho na kesho kutwa tutaambiwa Tanzania wana Corona Asilimia 50 wakati Tanzania hatuna Corona" alisistiza RC Shigela.
Katika hatua nyingine RC Shigela ameutaka uongozi wa Wilaya ya Mkinga kutenga eneo maalum la biashara ya kuuza nafaka mpakani kwa Mataifa yote mawili ili kuepusha Magari kusafiri umbali mrefu na kusaidia kupunguza usumbufu kwa Madereva na Wafanyabiashara wanaopeleka bidhaa zao nchini Kenya.
"Tumetembelea maeneo ya huu Mpaka, niombe Mkuu wa wilaya atenge eneo maalum la biashara za Nafaka hapa, Mtu wa Tanzania alete mahindi hapa, Mkenya anunue hapahapa" alisema Martin Shigela
No comments:
Post a Comment