Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Godfrey Ndalahwa (katikati). akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu mkutano mkuu wa 18 wa mwaka wa wanahisa wa benki hiyo unaotarajia kufanyika jijini Dar es Salaam Juni 27 mwaka huu. Kushoto ni Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Deogratius Thadei na Mkurugenzi wa Sheria na Katibu wa Kampuni, Regina Mduma.
Na mwandishi wetu, Dar
Takriban wanahisa 7,000 wa Benki ya DCB wanatarajiwa kufanya Mkutano Mkuu wa Mwaka Jumamosi ya Juni 27 mwaka huu kwa njia ya mtandao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Godfrey Ndalahwa, amesema hiyo itakuwa ni mara ya kwanza kwa mkutano huo kufanyika kidijitali.
“Ninawakaribisha wanahisa wote katika mkutano huo utakaoanza saa nne asubuhi, utakaotoa fursa kwa Benki na wanahisa kutathimini mkakati wa miaka mitano tuliojiwekea,” anasema Ndalahwa.
Hatua ya mkutano mkuu kufanyika kidijitali, mbali na kusababishwa na uwepo wa ugonjwa wa corona, imewezeshwa kutokana na uimara wa kitengo cha teknolojia ndani ya DCB.
Ndalahwa anasema mkakati huo uliopitishwa na kuanza kutekelezwa mwaka 2018, unatarajiwa kukamilika mwaka 2022.
“Mkakati huu una hatua tatu; kwanza kuiondoa benki katika kutengeneza hasara na kuanza kupata faida, pili benki kujiimarisha na tatu na kukukua na kutanuka kwa Benki ya DCB,” anasema.
Tayari mafanikio ya mkakati huo yameshaoneka kwani katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji wake, mwaka 2018 benki ilipata faida ya Sh bilioni 1.6 kutoka katika hasara ya Sh bilioni -6.5 mwaka 2017.
Mwaka 2019 DCB imepata faida ya Sh bilioni 2.1 kutoka Sh bilioni 1.6 ya mwaka 2018 huku thamani ya uwekezaji ikiongezeka:
“Hivyo kutoa nafasi kwa wanahisa kupata gawio kutokana na uamuzi watakaoufikia Jumamosi, Pia kutokana na mkakati huu, ukwasi umeongezeka huku mikopo chechefu ikipungua ikiwa ni katika hatua ya pili ya mkakati, yaani kujiimarisha.” Ndalahwa amesema.
Katika hatua ya tatu ya kujipanua, Benki ya DCB imefungua vituo 28 mikoa mbalimbali nchini na inatarajia kufungua matawi matano kwenye mikoa ya kimkakati kiuchumi nchini.
“Ninaamini wanahisa, pamoja na kujiadili gawio linalotokana na faida iliyopatikana; bado wanatamani kuiona benki yao ikiimarika na kuwafikia Watanzania wengi zaidi hivyo kusaidia juhudi za serikali za kuifikisha nchi yetu katika uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025,” anasema Mkurugenzi Mtendaji huyo.
No comments:
Post a Comment