Taarifa hiyo imetolewa leo Jumamosi tarehe 9 Mei 2020 jijini Dar es Salaam na Profesa Yunus Mgaya, Mkurugenzi Mkuu NIMR, wakati akizungumza na wanahabari.
Prof. Mgaya ameyataja magonjwa hayo kuwa ni, kisukari, shikizo la damu, Virusi vya Ukimwi (VVU), saratani na ugonjwa wa moyo.
Mwanzoni mwa mwezi Aprili 2020, Dk. Faustine Ndugulile, Naibu Waziri wa Afya, aliwataja wenye magonjwa hayo, kuwa katika hatari ya kupoteza maisha kutokana ugonjwa huo na Covid-19, na kuwataka wazingatie ushauri unaotoka kwa watalaamu wa afya.
Kufuatia tahadhari hiyo, Prof. Makubi amesema katika utafiti wa NIMR, taasisi hiyo inatafiti matatizo yanayopelekea wenye magonjwa hayo kuathirika zaidi, ikiwemo baadhi yao kupoteza maisha.
“Tunangalia wenye magonjwa hayo kama wakiwa na maambukizi wanakuwa na matatizo gani, kwa hiyo tuna utafiti ambao unaendelea, unaoangalia wagonjwa hao ili kuona wanaathirika kiasi gani kwa corona,” amesema Prof. Mgaya.
Prof. Mgaya amefafanua kuwa, wagonjwa hao wakipata maambukizi ya Covid-19 wanashindwa kupambana nao kutokana na kinga zao za mwili kuwa ndogo. Hivyo wanaofariki dunia, hawapotezi maisha kwa sababu ya Corona, bali kutokana na maradhi yao yaliyokuwepo awali.
“Tunafahamishwa kwamba kuna wananchi wana magonjwa yasiyo ya kuambukizwa, kinga zao za mwili zinashuka, kwa hiyo wakipata corona wanafariki kwa hayo magonjwa na si corona,” amesema Prof. Mgaya.
Wakati huo huo, Prof. Mgaya amesema NIMR inafanya tafiti takribani tisa kuhusu ugonjwa huo, ikiwemo utafiti kubaini mwenendo wa maambukizi ya Covid-19, na namna wananchi wanavyotekeleza ushauri wa kitaalamu juu ya kujikinga nao.
“Kama taasisi tumejikita katika tafiti tisa tayari, ambazo ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji, na lengo kubwa kupata majibu katika masuala mbalimbali ambayo sisi tunajiuliza na wanaohudumia wagonjwa wanashuhudia na haya majibu tutayapata baada ya utafiti,” amesema Prof. Mgaya.
Prof. Mgaya amesema taasisi hiyo itakapokamilisha tafiti hizo, itatoa matokeo yake kwa umma.
No comments:
Post a Comment