Klabu ya Yanga imelazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na Township Rollers ya Botswana katika mchezo wa kwanza Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Yanga SC inayofundishwa na kocha Mwinyi Zahera raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) sasa inakabiliwa na zoezi la kwenda kuupanda mlima wiki ijayo mjini Gaborone kwa kulazimisha ushindi wa ugenini, au sare ya kuanzia 2-2 ili isonge mbele kwa faida ya mabao ya ugenini.
Leo Yanga SC ilitanguliwa kwa bao la dakika ya saba tu lililofungwa na Phenyo Serameng, kabla ya kiungo Mnyarwanda, Patrick Sibomana kuisawazishia ‘Timu ya Wananchi’ dakika ya 86.
Serameng alifunga bao hilo baada ya kumpindua beki wa kushoto wa Yanga SC, Muharami Issa ‘Marcelo’ kufuatia pasi ya Kanogelo Matsabu na kufumua shuti la kiufundi kwa mguu wake wa kushoto kumtungua kipa mpya, Metacha Boniphace Mnata aliyesajiliwa kutoka Mbao FC ya Mwanza.
Kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Patrick Sibomana alipoteza nafasi ya kuifungia bao Yanga SC dakika ya 30 baada ya mkwaju wake wa penalti kupanguliwa na kipa Wagarre Dikago.
Penalti hiyo ilitolewa na refa George Gatpgato kutoka Burundi baada ya mpira uliopigwa na kiungo Mapinduzi Balama kumgonga beki wa Township Rollers, Ofentse Nato kwenye boksi.
Yanga SC wakapata pigo dakika ya 39 baada ya beki wake wa kulia, Paul Godfrey ‘Boxer’ kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na mchezaji mpya, Ally Ally aliyesajiliwa kutoka KMC.
Ofentse Nato tena akaunawa mpira kwenye boksi alioruka kichwa cha mkizi kuokoa krosi ya Issa Bigirimana kutoka upande wa kulia na Sibomana akaenda kuifungia Yanga bao la kusawazisha dakika ya 86.
Timu hizo zitarudiana Jumamosi ijayo Uwanja wa Taifa mjini Gaborone, Botswana na mshindi wa jumla atakutana na mshindi wa mechi kati ya Green Mamba ya Eswatini na Zesco ya Zambia.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Metacha Mnata, Paulo Godfrey/Ally Ally dk39, Muharami Issa, Ally Mtoni, Lamine Moro, Papy Tshishimbi, Mapinduzi Balama, Mohammed Juma, Sadney Urikhob, Juma Malinya/Issa Bigirimana dk68 na Patrick Sibomana/Mrisho Ngassa dk74.
Township: Wagarre Dikago, Maano Ditshupo, Kamogelo Matsabu, Ofentse Nato, Thatayaone Ditlhokwe, Kaone Vanderwesthuizen, Motsholetshi Sikele/Edwin Moalosi dk85, Mothusi Cooper, Segolame Boy, Tumisang Orebonye, Phenyo Serameng/Arnold Mampori dk69.
Post Top Ad
Your Ad Spot
Saturday, August 10, 2019
Yanga yatoa sare na Township Rollers uwanja wa Taifa
Tags
MICHEZO#
Share This
About kilole mzee
MICHEZO
Labels:
MICHEZO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment