LICHA ya wengi kuamini kwamba Simba itafanya vizuri msimu huu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Patrick Aussems ametoa kauli ambayo inaweza kutopokelewa vizuri na mashabiki wa timu yake.
Msimu uliopita, Simba ilifika robo fainali ya michuano hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kufikia mafanikio hayo, hali ambayo wengi wanaamini msimu huu itafanya vizuri ikiwemo kutwaa ubingwa kutokana na ubora wa kikosi cha timu hicho.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Aussems amefichua kile kilicho moyoni mwake kuwa licha ya kujitahidi kufanya usajili mzuri lakini haoni nafasi ya timu hiyo kuweza kuchukua ubingwa wa michuano hiyo kwa kuwa bado wanahitaji uzoefu mkubwa kwenye michuano hiyo.
“Nadhani suala la kuchukua ubingwa wa Afrika halipo katika malengo yangu, hiyo ni kwa sababu siyo kitu rahisi, haya mashindano yanashirikisha timu nyingi kubwa na zina uzoefu mkubwa tofauti na sisi.
“Kitu kikubwa kwetu ambacho kinapaswa kueleweka kwamba, tunahitaji kwanza tupate uzoefu wa kutosha, msimu uliopita tumefika robo fanali inawezekana msimu huu tusifike kabisa huko, kitu cha muhimu kwetu ni kuweka malengo ya kushiriki sana kwa kuchukua ubingwa wa ndani lakini siyo kuchukua ubingwa wa Afrika,” alisema Aussems.
No comments:
Post a Comment