Wananchi wenye hasira kali wamemuua kisha kumchoma moto Juma Lugomba mwenye umri wa miaka 61, Mkazi wa Kijiji cha Chiwata Kata ya Chiwata Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara, baada ya Juma kudaiwa kumshambulia Mkewe kwa shoka na kumuua jambo lililosababisha Wananchi hao kupandwa na hasira na kumuadhibu.
Tukio hilo limetokea katika kijijini Chiwata, na limethibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Selemani Mzee ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.
Mzee alisema inadaiwa juzi saa 3 usiku, Lugomba alimshambulia mkewe Yolenda Milanzi (59) na kitu chenye ncha kali na kumsababishia majeraha yaliyopelekea kifo baada ya kumjeruhi vibaya kichwani.
Alidai mkazi huyo baada ya kufanya mauaji hayo kwa mkewe, kundi la wananchi wenye hasira kali waliamua kumsaka na walipomkamata walimjeruhi kisha kumchoma moto hadi kusababisha kifo chake na yeye.
“Ni kweli tukio hilo limetokea mume kumshambulia mke wake na kumuua, lakini baada ya yeye kufanya mauaji hayo asubuhi yake wananchi waliamua kumsaka na walipomkamata walimjeruhi kisha kumchoma moto hadi kufa,” alieleza DC huyo.
Alisema bado chanzo cha mume huyo kufanya mauaji kwa mkewe hakijafahamika, lakini Polisi wanaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo.
Mtendaji wa Kijiji cha Chiwata, Thawabu Mturi alisema mume huyo baada ya kufanya mauaji, alikimbilia kijiji cha jirani cha Pemba kujificha ili kukwepa ushahidi.
Alisema wananchi walipogundua kuwa mume huyo amemuua mke wake, walipandwa na hasira ndipo walipoamua kumtafuta wakiwa na wabeba silaha za kijadi na walipogundua kuwa amejificha katika kijiji jirani walifika huko na walifanikiwa kumkamata hivyo walimjeruhi kisha walimchoma moto hadi kufa.
No comments:
Post a Comment