Wakati sakata la wakurugenzi wa halmashauri za Wilaya, miji na majiji kusimamia uchaguzi likiendelea kushika kasi, Rais Mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume, amesema hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda wa Dar es Salaam haijawapiga marufuku viongozi hao kusimamia uchaguzi wa madiwani.
Akizungumza, Fatma alisema wakurugenzi hao hawajapigwa marufuku kwa sababu uchaguzi wa madiwani unafanyika chini ya Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa tofauti na Sheria ya Taifa ya Uchaguzi inayosimamia uchaguzi wa rais na wabunge ambayo ndiyo Mahakama Kuu ilipiga wateule hao wa Rais kusimamia.
Kauli hiyo ya Fatma imekuja siku chache baada ya Juni 2 mwaka huu vyama vinane vya upinzani kutishia kutoshiriki uchaguzi wa marudio katika kata 32 unaotarajiwa kufanyika Juni 15 endapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hakitatekeleza hukumu hiyo ya Mahakama.
Akifafanua katika hilo, Fatma alisema kuna sheria mbili zinazosimamia chaguzi nchini ikiwamo Sheria ya Taifa ya Uchaguzi inayosimamia uchaguzi wa Rais na wabunge na pamoja na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambayo inahusu uchaguzi wa madiwani na viongozi wengine wa serikali za mitaa.
“Uamuzi wa Mahakama Kuu umelenga uchaguzi wa Rais na wabunge kwa sababu wao hawachaguliwi chini ya National Election Act (Sheria ya Taifa ya Uchaguzi), hawa wengine wanachaguliwa chini ya Local Election Act (Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa).
“Sasa Local Election Act bado haijapigwa marufuku. Kile kifungu kinachoruhusu ma-DED kuwa wasisimizi wa uchaguzi kwenye Local Election Act hakijapigwa marufuku kwenye National Election Act Mahakama imeshapiga marufuku kile kifungu.
“Tatizo ni hivi, kwamba serikali kwa sababu Mahakama Kuu imeshasema kwamba ile sheria ya National Election Act haifuati Katiba, ina wajibu wa kutazama sheria zote nyingine zilizokuwa kama hii ili izibadilishe bila watu kwenda mahakamani. Huo ndiyo wajibu wa Serikali,” alisema Fatma.
Kuhusu kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Aderladus Kilangi, kuwa baada tu ya serikali kuwasilisha kusudio la kukata rufaa kupinga utekelezaji wa hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa Mei 10 mwaka huu kuwazuia wakurugenzi kusimamia uchaguzi, kwamba utekelezaji wa hukumu hiyo unasimama hadi pale rufaa ya serikali itakapoamriwa, Fatma alisema kusudio hilo halizuii kutekelezwa kwa hukumu hiyo.
“Haizuii kabisa hukumu ya Mahakama kutekelezwa, hukumu ya Mahakama haiwezi kuachwa kutekelezwa kwa sababu Kilangi kakata rufaa. Lakini vilevile hii kesi haijahusu local election (Uchaguzi wa Serikali za mitaa) inahusu National election (uchaguzi wa kitaifa).
“Uchaguzi unafanyika chini ya sheria tofauti, hata kama unafanyika siku moja lakini unafanyika kwa sheria tofauti. Ni kama Zanzibar kuna chaguzi kama tatu hivi zinafanyika siku moja, unafanyika uchaguzi wa Rais na Baraza la wawakilishi Zanzibar chini ya sheria nyingine, uchaguzi wa madiwani sheria nyingine na uchaguzi wa wabunge na Rais wa Tanzania kwa sheria nyingine,” alisema Fatuma.
No comments:
Post a Comment