Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii.
SHAHIDI wa pili katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa analichukia jeshi la polisi kuanzia siku alipoona video kwenye mtandao wa kijamii wa you tube ikimuonyesha Zitto Kabwe akielezea polisi wanavyowatendea ukatili raia.
Shahidi huyo Mashaka Juma ambaye ni msanii wa filamu, akiongozwa na Wakili wa serikali Mkuu Tumaini Kweka kutoa ushahidi wake, amedai, Oktoba 29,2018 huko Kimara Korogwe akiwa na wenzake wakicheza drafti alifika rafiki yao, Frenky Zong na kuwauliza kama wamepata habari yeyote ambapo wao hawakuwa na taarifa.
"Zong alitutolea simu yake kisha akatufungulia na tukaangalia habari kwenye yuotube ambapo tulimuona Zitto akililaumu jeshi la polisi kwa mambo mbalimbali ambayo wameyafanya wilayani Uvinza Mkoa wa Kigoma," amedai.
Ameendelea kudai kuwa, kwenye video hiyo Zitto anaonekana akieleza jinsi jeshi la polisi linavyowanyanyasa wananchi, kuteka watu akiwemo Mo wa Simba na jinsi walivyoenda hospitali kuwateka watu waliokuwa wakitibiwa na kwenda kuwaua na pia video hiyo inamuonyesha Zitto akielezea jinsi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini alivyoshindwa kuwadhibiti askari wake .
Shahidi huyo amedai kuwa, alipoona video ile na taarifa aliyotoa Ziito ambaye anamfahamu kwa muda mrefu, aliona jeshi la polisi halina thamani kama wameshindwa kulinda raia na mali zake ndipo alipolichukia hadi leo jeshi hilo.
Katika kesi , Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi anayodaiwa kutenda, Oktoba 28,2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama cha ACT Wazalendo.
No comments:
Post a Comment