Daktari Bingwa Upasuaji (plastic surgery), Dkt. Ibrahim Mkoma wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu huduma ya matibabu ambayo Bi. Mariam Rajab Juma ameanza kupatiwa katika hospitali hiyo.
Na John Stephen Massawe.
Wataalam wabobezi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), leo wameanza kufanya vipimo mbalimbali vya uchunguzi kwa Mariam Rajab Juma mwenye kidonda sehemu ya mgongoni ili kubaini chanzo cha ugonjwa alionao.
Akizungumza na Wanahabari juu ya mwenendo wa matibabu ya Mariam, Daktari Bingwa wa Upasuaji Dkt. Ibrahim Mkoma amesema vipimo hivyo ni pamoja na kuchukuliwa sampuli ya nyama kutoka sehemu ya kidonda na kupelekwa maabara kwa watalaam wa patholojia ili kubaini kama kuna saratani au la.
Aidha Mariam ameandikiwa kufanya vipimo mbalimbali ikiwemo CT-scan ya kifua na kichwa, Ultrasound pamoja na vipimo mbalimbali vya damu.
Dkt. Mkoma amesema kidonda kilichopo sehemu ya mgongo wa Mariam ni kidonda sugu na kwamba hadi sasa haijabainika kama mgonjwa huyo ana tatizo la saratani au la mpaka hapo majibu ya wapatholojia yatakapo patikana ndani ya siku nne kuanzia sasa.
Mariam amesema aliwahi kuugua moto akiwa na umri wa miaka mitano ambapo alitibiwa na kupona ingawa alibaki na kovu kubwa kuanzia sehemu ya mgongo wake hadi kwenye kisogo.
Amesema mwezi wa nane mwaka jana alipata kipele kwenye kovu na baadae kipele hicho kugeuka kuwa jipu. Alipotumbua jipu lilitoa usaha na kisha kuanza kuota kidonda kilichoendelea kuongezeka siku hadi siku.
“Nilienda kutibiwa katika Hospitali ya Makiungu iliyopo Manispaa ya Singida, lakini pia kutokana na wazazi wangu kutokua na uwezo wa kifedha niliacha kwenda hospitalini na kuanza kusafisha kidonda mwenyewe, huku nikiwaomba marafiki zangu niliosoma nao sekondari wanichangie fedha ili niweze kununua dawa,” amesema Mariam.
Amesema wakati anatibiwa katika Hospitali ya Makiungu wataalam walimshauri kuja Muhimbili ili kupatiwa matibabu zaidi, lakini kutokana na wazazi wake kukosa fedha alimtafuta rafiki yake aitwaye Seif ambaye pia alisoma naye sekondari akamrekodi kwa simu yake na kutuma kwenye mitandao ya kijamii na huo ukawa mwanzo wa yeye kuanza kupata msaada.
Mariam anaishukuru Serikali kupitia kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na Menejimenti ya Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuitikia wito wa kumsaidia na kuanza kumpa huduma.
Aidha, anawashukuru Watanzania kwa jinsi walivyompigia simu na kutaka kumsaidia baada ya kuona picha ya video kwenye mitandao ya kijamii.
Habari kwa hisani ya Muhimbili National Hospital
No comments:
Post a Comment