Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza haja ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zambia.
Dk. Shein aliyasema hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Zambia Hassan Simba Yahya ambapo mazungumzo hayo yalijikita zaidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya pande mbili hizo.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi Hassan Simba kuwa historia iliopo kati ya pande mbili hizo ni vyema ikaimarishwa kwa kuendeleza sekta za kiuchumi na maendeleo hasa katika kutekeza Sera ya Diplomasia ya Uchumi.
Dk. Shein alimueleza Balozi huyo azma ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutekeleza Sera ya Diplomasia ya uchumi ikiwa ni pamoja na kuhamasisha uwekezaji hasa katika sekta ya viwanda kwani ndio kiu ya uchumi wa Tanzania hivi sasa.
Alieleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zambia zimekuwa zikishirikiana katika nyanja mbali mbali hasa ikizingatiwa kuwa nchi mbili hizo ni wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Bara la Afrika (SADC).
Rais Dk. Shein alisema kuwa kwa vile Tanzania hivi sasa ndiye Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, ni vyema mkazo zaidi ukawekwa katika kuhakikisha mashirikiano ya nchi wanachama wa Jumuiyahiyo yanaimarika zaidi kwa azma ya kufikia malengo yaliyowekwa.
Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zambia zina uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu ambao umesababisha watu wa pande mbili hizo kuishi kama ndugu hasa kwa kuwepo kwa mradi mkubwa wa usafiri wa Shirika la Reli ya pamoja kati ya Zambia na Tanzania (TAZARA).
Dk. Shein alieleza kuwa uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Zambia na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni njia moja ya kuimarika zaidi kwa mahusiano ya wananchi wa pande mbili hizo hasa ikizingatiwa kuwepo kwa usafiri wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).
No comments:
Post a Comment