Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, inakamilisha taratibu za kidiplomasia ili kuwezesha Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), kuanza safari za moja kwa moja kwenda India na China.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mawasiliano, Ujenzi na Uchukuzi, Isack Kamwelwe, wakati wa mahafali ya kwanza ya wahudumu wa ndani ya ndege katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Amesema taratibu hizo baina ya serikali ya mataifa hayo, zitakamilika karibuni. Alisema kutokana na hatua hiyo, safari hizo zinatarajiwa kuanza mwisho wa mwezi huu au mwanzoni mwa mwezi ujao hasa nchini India.
Waziri huyo pia alieleza kuwepo kwa mikakati mbalimbali ya kuwezesha ndege za ATCL kwenda katika mataifa mbalimbali ikiwemo nchi za Ulaya.
Amesema katika kuhakikisha wanaliboresha zaidi shirika hilo, serikali ilitenga Sh bilioni 900 ambazo zimeelekezwa katika ununuzi wa ndege.
Amesisitiza kuwa kutokana na jitihada hizo, uwepo wa kada hiyo ya watoa huduma wa ndani ya ndege ni muhimu huku akiipongeza NIT kwa kuanzisha kozi hiyo.
"Tunatarajia hadi itakapofika mwishoni mwa mwezi wa tano ndege zetu zitaanza kuruka kwenda nchini China, pamoja na hilo serikali pia imekuwa ikiendelea na ujenzi wa viwanja mbalimbali nchini, lengo ni kuhakikisha tunaliwezesha shirika letu kukua siku hadi siku," alisema Kamwelwe.
Aidha, Kamwelwe alisema NIT ina jukumu kubwa la kuhakikisha kinazalisha wataalamu wa kutosha, watakaotoa msaada katika kuliendeleza shirika hilo na hivyo kukabiliana na uhaba uliopo nchini hivi sasa.
No comments:
Post a Comment