Na John Walter-Babati
Mbunge wa jimbo la Babati mjini [CCM] Paulina Gekul amesema katika bunge lijalo la bajeti watamshauri waziri wa Afya Ummy Mwalimu aruhusu bima kubwa ya shilingili 76,800 inayotolewa kwenye vikundi pekee itolewe kwa mtu mmoja mmoja na sio kwenye vikundi.
Gekul anasema hilo walishamweleza waziri Ummy ambaye alisema kuwa amepokea maoni hayo na atayafanyia kazi ila ikiwezekana inabidi zitolewe kwa kuzingatia umri wa mtu kwa sababu kadri umri unavyopanda na magonjwa ndiyo yanazidi.
Gekul amesema mwananchi anapokuwa na Bima kubwa ya afya itakuwa ni rahisi kupata huduma za matibabu katika hospitali yeyote hapa nchini tofauti na ya shilingi 30,000 ya sasa inayoruhusu kutibiwa katika hospitali ndani ya mkoa husika.
Kumbuka kwa mtu ambaye siyo mwajiriwa wa serikali au sekta rasmi binafsi anaweza kupata huduma kupitia kikundi kilichosajiliwa kwa kuchanga Shilingi 76,800 kwa mtu mzima wakati watoto wanachangia Shilingi 50,400.
"Mimi kwenye pochi yangu naweza kusahau kadi ya benki lakini bima ya afya siwezi kuisahau,kina mama tunapenda familia zetu bima ni elfu 30,usikae nyumbani bila kuwa na bima inasiadia sana"alisisitiza Gekul
Amesema ni furaha yake kuona kila mwananchi wa jimbo la Babati mjini anakuwa na uhakika wa kupata huduma za afya kwa nyakati zote bila kujali kipato chake, kwa kuwa unapokuwa na huduma hizo hata kazi za maendeleo hufanyika kwa ufanisi.
Amesema kuna watu wanateseka wanapopatwa na maradhi wakati hawana pesa haswa katika kipindi hiki ambacho ni cha masika,pesa zinakwenda kulipa mahitaji ya wanafunzi hivyo bima itarahisisha na kuondoa ugumu wa kupata matibabu.
Mbunge huyo amesema ni muhimu kuwa na bima ya afya kwani unapoumwa ni suala linalogusa uhai na bila hivyo utaugua na hata kufa kwa kukosa matibabu.
No comments:
Post a Comment