Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka wazi kuwa suala la kutangaza nyongeza za mishahara kwa watumishi wa umma hadharani husababisha athari kwa jamii nzima na kwa wale ambao siyo watumishi.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akiwa bungeni kwenye kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge Suzani Lyimo aliyehoji ni kwa nini serikali ya awamu ya tano inakiuka sheria ya utumishi wa umma ya kutoa nyongeza kwa watumishi wake.
Mh. Majaliwa amesema kwamba siyo kwamba serikali haikusudii kuongeza mshahara kwa watumishi wake lakini kutumia siku kama Mei 1 kutangaza nyongeza za mishahara husababisha athari kwa wananchi wote kwani vitu vinaweza kupanda bei na kusababisha usumbufu kwa watu wengine wasiopokea mishahara.
Pamoja na hayo, Mh Majaliwa ameeleza kuwa "Suala la mshahara ni siri ya mtu. Siyo lazima litangazwe hadharani. Ndiyo maana hata tunapolipa madeni hatutangazi lakini wanaodai wanaona kwenye mishahara yao kwamba malipo yanaingia. Lengo la serikali ni kupunguza na gharama za maisha".
Ameongeza "Serikali ina utaratibu wa kuwapa stahiki watumishi kadiri inavyotakiwa na inaratibiwa vizuri. Tunaendelea na uboreshaji wa maeneo hayo kama nyongeza za mshahara, na upandishaji wa wa madaja. Watumishi wawe na imani na serikali. Rais alitenga zaidi ya bilioni 200 na tumeshaanza kulipa madeni. Nyongeza za mishahara zitatolewa kwani Rais alikwisha ahidi"
No comments:
Post a Comment