A great place to access the latest news and information.

Breaking

Post Top Ad

Your Ad Spot

Saturday, June 9, 2018

Mfumo Mpya wa Malipo Mamlaka za Serikali za Mitaa Kuboresha Huduma kwa Wananchi.

Mkufunzi wa mafunzo ya mfumo wa malipo Epicor toleo Na. 10.2 kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. Augustino Manda (aliyesimama) akitoa maelezo ya awali ya mafunzo hayo kwa Maafisa Manunuzi kutoka Halmashauri za Mikoa ya Dodoma, Singida, Shinyanga, Arusha na Manyara , leo Jijini Dodoma.


Na: Lilian Lundo  MAELEZO, Dodoma.


Mfumo mpya wa malipo epicor toleo Na. 10.2 unaotarajiwa kuanza kutumika Julai 1 mwaka huu na Mamlaka zote za Serikali za Mitaa nchini umeelezwa kuboresha huduma kwa wananchi kutokana na kuwa wa uwazi na kurahisisha kazi kwa watumiaji wa mfumo huo.

Akieleza lengo la uboreshaji wa mfumo huo leo, Jijini Dodoma wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Manunuzi kutoka Halmashauri za Mikoa ya Kigoma, Shinyanga, Dodoma, Arusha, Manyara na Singida, mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Agustino Manda amesema mfumo huo utapunguza kazi na kuongeza ufanisi wa kazi kwa watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa hapa nchini.

Mfumo huu utaweka mambo wazi, watu watawajibika na mtumiaji wa mwisho ambaye ni mteja atapata huduma nzuri na kuridhika na huduma atakayopewa, amesema Manda.

Ameendelea kusema, lengo la kuboresha mfumo huo ni kutoa huduma nzuri kwa Wananchi, Wananchi kutocheleweshewa huduma,  Halmashauri husika kuwa katika nafasi nzuri ya kutoa huduma  pamoja na kukusanya mapato vile ilivyotarajiwa.
Aidha amewataka Maafisa Manunuzi hao kutoa maelekezo mazuri kwa wateja wao  namna mfumo huo unavyofanya kazi ili wateja waweze kuelewa na kuridhika na huduma wanazohitaji.

Manda amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3)  kupitia mifumo mbalimbali ya kielektroniki inayoendelewa kuboreshwa hapa nchini wamefanikiwa kupunguza gharama za watumishi kusafiri  kwenda Makao Makuu ya Serikali kufuata huduma mbalimbali.

Ametolea mfano wa Mfumo wa Kielektroniki wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali za Mitaa (PlanRep) kuwa umewezesha Halmashauri kuandaa bajeti zao wakiwa katika ofisi zao tofauti na awali, ambapo walilazimika kusafiri kwenda Dar es Salaam au Dodoma.

 Hivyo mradi huo umeipunguzia Serikali gharama za kuwalipa watumishi hao wanapokuwa nje ya vituo vyao vya kazi.

Kwa upande wa Meneja  Mradi wa PS3 Dodoma,  Bw.  Gideon Muganda amesema PS3 itaendelea kushirikiana na Serikali kwa ukaribu kuhakikisha mifumo mbalimbali ya sekta za Umma inaboreshwa hapa nchini.

Mfumo wa malipo epicor 10.2 utatoa taarifa zote zinazohusiana na fedha katika Halmashauri husika ikiwemo mapato, matumizi pamoja na bajeti ya Halmashauri.

Mafunzo ya Mfumo huo yanaendelea kutolewa katika vituo sita ambavyo ni Dodoma, Mwanza, Mtwara, Iringa, Kagera na Mbeya ambapo yamehusisha  watumiaji wa mfumo huo ambao ni Waweka Hazina, Wahasibu, Maafisa TEHAMA, Maafisa Manunuzi na Wakaguzi wa Ndani kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini lengo ikiwa ni kuwajengea uwezo wa namna ya kutumia mfumo huo hasa katika maeneo yaliyoboreshwa.

Mafunzo hayo yanafanyika kwa wiki tatu ambapo yameanza  Juni 4  na yanatarajiwa kumalizika Juni 21, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages